He! Zahera ashtukia kitu kwa Ndanda

Muktasari:

  • Zahera alisema mbali na kukutana na nyota hao katika mzunguko wa kwanza wametumia vipande vya baadhi ya michezo waliyocheza ili aweze kufahamu mabadiliko ya timu hiyo yalipo na wayafanyie kazi mapema kabla ya mchezo.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema hakuna mchezo mwepesi kwao na kuweka wazi kuwa wanatarajia kukutana na ugumu kwenye mchezo wa leo Alhamisi dhidi ya Ndanda FC kutokana na timu hiyo kuwa katika nafasi mbaya kwenye msimamo.

Ndanda ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza michezo 29 na kufikisha pointi 36 inatarajia kucheza na Yanga katika uwanja wake wa nyumbani ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya bao 1-1 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema kikosi chake kipo katika hari nzuri ya ushindani na anategemea kuibuka na ushindi katika mchezo huo na kuweka wazi kuwa hategemei mteremko kwani anawaheshimu wapinzani wake.

“Ndanda ni timu nzuri ilitupa wakati mgumu nyumbani, hivyo sio rahisi sisi kupata matokeo katika uwanja wao wa nyumbani lakini ninachoweza kuwaambia mashabiki na Watanzania wanaoipenda timu hii wategemee ushindi kwani tumejiandaa kushindana sio kukubali kushindwa.

“Ubora na ugumu wa ligi unaanzia mzunguko wa pili tunakutana na timu ambayo haipo katika nafasi nzuri kwenye msimamo inapambana kupanda na sisi tunatafuta nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi na kuendelea kujikita kileleni kwenye msimamo,” alisema.

Alisema Ndanda ipo nafasi ya 14 lakini pointi zake hazijaachana sana na timu ambazo zipo katika hatari ya kushuka daraja, hivyo wanatarajia kupata ugumu katika mchezo huo japo ametambia nyota wake kuwa wapo katika hari nzuri ya ushindani.

Zahera alisema mbali na kukutana na nyota hao katika mzunguko wa kwanza wametumia vipande vya baadhi ya michezo waliyocheza ili aweze kufahamu mabadiliko ya timu hiyo yalipo na wayafanyie kazi mapema kabla ya mchezo.

Mara ya mwisho Yanga kupata matokeo katika uwanja huo ilikuwa ni msimu uliopita ambapo mwiko huo ulivunjwa kutokana na ushindi wa mabao 2-1 iliyoupata katika mchezo wa raundi ya 19 ya ligi hiyo, ikiwachapa Wana-Kuchere kwa mara ya kwanza katika uwanja huo.