He! Kroos sasa anamtafuta ubaya kocha wake Madrid

Muktasari:

Kwa sasa kocha Lopetegui amemrudisha Kroos nyuma kucheza kwenye eneo la kukaba sambamba na Mbrazili, Casemiro.

MADRID, HISPANIA.Toni Kroos ametibuana na kocha wake Julen Lopetegui huko Real Madrid juu ya mbinu zake huku kiungo huyo mchezeshaji akimwambia kocha wake “Mimi sio Casemiro”.

Mjerumani huyo amekuwa kwenye kiwango bora kabisa huko Los Blancos akipewa uhuru wa kucheza anavyotaka kwenye sehemu ya kiungo, lakini tangu ujio wa kocha Lopetegui kila kitu kimebadilika na staa huyo wa zamani wa Bayern Munich anapangwa kwenye kiungo ya chini zaidi, eneo ambalo hataki kwa sababu hawezi kuwezi kuonyesha makali yake.

Kroos anataka kucheza kwenye eneo la karibu na goli la mpinzani kwa sababu anakuwa hatari zaidi anapokuwa na mpira kwenye eneo hilo kwa sababu pasi zake za mwisho zimekuwa dhahabu hata huko kwenye timu yake ya taifa ya Ujerumani.

Kroos kucheza kwenye eneo hilo jipya kwa msimu huu limedaiwa huenda limeshangia kwa kiasi kikubwa kwa timu hiyo kucheza mechi nne mfululizo bila ya ushindi, lakini si kushinda tu hata bao imeshindwa kufunga.

“Ni changamoto ambayo tunapaswa kuifanyia kazi. Siku zote kumekuwa na mambo kama haya, hivyo huwa hayanishtui. Napenda kucheza chini, lakini ifahamike tu mimi sio Casemiro.”

Kroos amecheza mechi 10 kwenye kikosi cha Madrid msimu huu, ikiwa ni mechi moja nyuma ya alizocheza Casemiro.