Hawauzwi hadi timu zao za zamani zielezwe

Muktasari:

Hata hivyo, Depay si mchezaji wa kwanza aliyeuzwa na mkataba wake kuwekwa kipengele cha kununuliwa tena na klabu yake ya zamani wakati timu hiyo mpya itakapofikiria kumuuza.

LONDON, ENGLAND . STAA wa Kidachi, Memphis Depay amekuwa mtamu huko Olympique Lyon na kuzifanya klabu kibao kupambana kunasa saini yake.

Lakini bosi wa Lyon, Juninho amefichua mchezaji huyo hawezi kuuzwa kwenda timu yoyote kabla ya kuwapa taarifa Manchester United kwanza kutokana na kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake.

Man United ilimnasa Depay kwa Pauni 25 milioni akitokea PSV Eindhoven mwaka 2015, ikampa jezi namba 7 kabla ya kumpiga bei miaka miwili baadaye kwenda Lyon kwa ada ya Pauni 16 milioni.

Wakati inamuuza, Man United ilitambua ubora wa mchezaji huyo na ndio maana imeweka kipengele hicho cha kupewa nafasi ya kwanza ya kumsajili mchezaji huyo wakati Lyon itakapotaka kumpiga bei. Tottenham Hotspur imedaiwa kwamba ipo tayari kutoa Pauni 50 milioni kumsajili mchezaji huyo, lakini sasa ni Man United ndio itakayoamua kwanza kama inamtaka au haimtaki kabla hajauzwa kwingineko.

Hata hivyo, Depay si mchezaji wa kwanza aliyeuzwa na mkataba wake kuwekwa kipengele cha kununuliwa tena na klabu yake ya zamani wakati timu hiyo mpya itakapofikiria kumuuza.

Mesut Ozil

Taarifa za Football Leaks zilifichua mwaka 2016 Arsenal italazimika kuwaambia Real Madrid kama itaamua kumpiga bei Mesut Ozil kwenda kwenye klabu nyingine ya Hispania. Hiyo ina maana Arsenal hawapaswi kumuuza Ozil kwenye timu yoyote ya Hispania kabla ya kuiambia Real Madrid kwanza kuamua kama ni wao watamsajili au wataruhusu uhamisho huo ufanyike. Real Madrid itakuwa na saa 48 za kufanya uamuzi na kama italipwa faida ya asilimia 30 kama Ozil atauzwa kwenye timu nyingine ya Hispania kwa dau la zaidi ya Euro 50 milioni.

Nathan Ake

Chelsea ilishakifanyia kazi kipengele kimoja ilichokuwa imekiweka kwenye mkataba wa beki Nathan Ake cha kumrudisha Stamford Bridge katikati ya msimu wakati alipokuwa akicheza kwa mkopo huko Bournemouth, Januari 2017.

Baada ya hapo, beki huyo alicheza mechi tano kwenye kikosi cha The Blues kabla ya Bournemouth kumbeba jumla Mdachi huyo kwa Pauni 20 milioni. Kiwango chake Ake kimekuwa moto kabisa akiwa mmoja kati ya mabeki wanaofanya vizuri kwenye Ligi Kuu England na kwamba Bournemouth ikiamua kumuuza itabidi Chelsea ipate taarifa kwanza.

Jadon Sancho

Moja kati ya makinda matata kabisa wanaotamba kwenye soka kwa sasa. Jadon Sancho amekuwa moto kwelikweli huko kwenye kikosi cha Borussia Dortmund kiasi cha kufanya thamani yake kufikia Pauni 100 milioni kama unahitaji thamani yake.

Kuna timu nyingi zinamtaka Sancho ikiwamo Manchester United ya Ligi Kuu England, lakini Dortmund haitaruhusiwa kumuuza winga huyo kabla ya kuiambia Manchester City kwanza. Dortmund itakachopaswa kufanya ni kuiambia Man City bei inayomuuza Sancho kuona kama wao watakuwa tayari kulipa, wakishindwa basi itakuwa ruhusu kumuuza kwingineko.

Jordon Ibe

Jurgen Klopp aliwaambia Liverpool wahakikishe wanaweka kipengele cha kuwa wa kwanza kumnunua mchezaji huyo tena wakati Jordon Ibe aliporuhusiwa kwenda kujiunga na Bournemouth kwa Pauni 15 milioni mwaka 2016.

Lakini, sasa miaka mitatu imepita na kiwango cha Ibe kwenye Ligi Kuu England kimekuwa si tishio sana jambo ambalo wala haliipi shida Liverpool kwamba huenda ikatokea timu nyingine itahitaji huduma ya mchezaji huyo na kuuzwa ghali wao wakashindwa kulipia. Ibe bado anakipiga huko kwenye kikosi cha Bournemouth na hajatokea mnunuzi na timu hiyo haijaamua kumuuza.

Adnan Januzaj

Kinda Adnan Januzaj aliibukia kwa kasi sana kwenye kikosi cha Manchester United na hakika alitabiriwa kufanya mambo makubwa. Lakini, baadaye mambo yalikuwa magumu akatolewa kwa mkopo kabla ya kuuzwa kwenda Real Sociedad mwaka 2017. Wakati inampiga bei, Man United ilitambua kiwango cha Januzaj huenda akaenda kuwa staa mmoja mkubwa sana duniani baada ya wakati fulani kugombewa na mataifa kibao wakitaka akacheze timu zao za taifa kabla ya kuamua kuitumikia Ubelgiji.

Man United ilimwekea kipengele cha kumnunua wao kwanza pindi mchezaji huyo atakapouzwa na timu yake ya sasa hiyo ni hofu kwamba asije kunyakuliwa na timu wapinzani wao wakati akiwa kwenye kiwango cha juu cha soka lake.

Bertrand Traore

Chelsea iliibwaga Manchester United kwenye usajili wa Bertrand Traore wakati ilipomnasa fowadi huyo kutoka Auxerre baada ya kumwona akitamba akiwa na kikosi cha Burkina Faso kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa chini ya miaka 17 huku yeye mwenyewe akiwa na umri wa miaka 14 kwa wakati huo. Mwaka 2016, mchezaji huyo alionyesha ubora wake wakati alipofunga mabao manne katika mechi tano na mwaka uliofuatia iliamua kumuuza kwenda Lyon baada ya kufanya vizuri kwa mkopo huko Ajax. Ilichokifanya Chelsea ni kuweka kipengele cha kupewa kwanza nafasi ya kumsajili Traore wakati Lyon itakapoamua kumuuza.

Kelechi Iheanacho

Leicester City ilifanikiwa kuinasa huduma ya Kelechi Iheanacho mwaka 2017 na kuzipiku klabu za Tottenham, West Ham na Monaco. Staa huyo alitokea Manchester City, ambako aliondoka na kuacha timu yake huko nyuma ikionyesha Liverpool ubabe na kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England mwaka uliofuatia.

Lakini, wakati inamuuza, Man City iliweka kipengele kwenye mkataba wake kwamba kwa vyovyote Iheanacho atakavyokuwa kwenye ubora, basi timu hiyo itakapohitaji saini yake basi itumie Pauni 50 milioni tu kumrudisha mchezaji huyo Etihad bila ya kujali thamani yake atakayokuwa nayo sokoni kwa wakati huo.

Yerry Mina

Barcelona si tu imekuwa maarufu kwa kuweka vipengele vya kutaka kuwanunua tena wachezaji wake, bali imekuwa ikikifanyia kazi vipengele hivyo wakati ilipowasajili Luis Garcia, Gerard Deulofeu na Denis Suarez kuwarudisha kwenye timu yao katika misimu ya karibuni.

Beki Yerry Mina, ambaye ameitumikia Barca mechi sita tu baada ya kujiunga nayo kwa ada ya Euro 11.8 milioni kutoka Palmeiras, naye amewekewa kipendele hicho alipouzwa kwenda Everton. Kwamba wababe hao wa Goodison Park watakapoamua kumuuza Mina au Barca watakapomhitaji basi waruhusiwe kumsajili kwa Pauni 54 milioni tu na si vinginevyo.

Memphis Depay

Jose Mourinho ndiye aliyefichua kwamba walitambua ubora wa mchezaji Depay na hivyo kuamua kuweka kipengele cha kumnunua kwanza wakati Lyon itakapotaka kumuuza Mdachi huyo.

Mourinho alisema kwamba anafahamu wazi Louis van Gaal alimsajili Depay wakati akiwa Man United kutokana na ubora wa mchezaji huyo na hisia ya kwamba atakwenda kuwa mchezaji mkubwa sana kwa miaka ya baadaye, hivyo hata wao walipoamua kumfungulia mlango wa kutoka basi waliweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wanapata nafasi ya kumrudisha Old Trafford watakapohitaji kufanya hivyo au Lyon watakapotaka kumuuza.

Jambo hilo linaifunga Lyon kumuuza Depay kwenye timu nyingine yoyote kabla ya kuipa taarifa Man United.