Hawa wa Diamond akwea pipa kwenda kutibiwa India

Saturday October 13 2018

 

By Nasra Abdallah

Dar es Salaam. Hatimaye msanii Hawa Said 'Hawa Diamond' amesafiri kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.

Hawa aliyeimba Diamond wimbo wa Nitarejea amesafiri leo kwenda katika matibabu hayo akisindikizwa na Mama yake Ndagina Hassana pamoja na Meneja wa Diamond, Babu Tale.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuondoka, Hawa aliwaomba Watanzania kumuombea dua katika matibabu hayo.

Naye mama yake Ndagina Shabani aliwashukuru watanzania kwa upendo walioonyesha kwa mtoto wake na kueleza kuwa hana cha kuwalipa kwani bila wao huenda hata msaada huo wa matibabu wasingeupata leo.

Naye meneja Babu Tale alisema wanatarajia kuwa nchini humo kwa wiki mbili na huenda Hawa akapandikizwa ini kama madaktari watashauri hivyo.

Alisema wamelazimika kumsaidia Hawa baada ya kuona hali yake kwenye vyombo vya habari na kuongeza kwamba watanzania wanapaswa kuwaunga mkono katika hilo kwani msanii huyo bado anahitaji matibabu na huduma nyingine zaidi.

"Kama mlivyoona hali ya Hawa sio ya kusema atapona mara moja anahitaji msaada wa watanzania wengi zaidi, sisi tumeanza basi na wengine wanaweza kujitolea kwa chochote kitu ili aweze kupona," amesema Babu Tale.

Hawa aliyewahi kutamba na wimbo wa 'Nitarejea' aliomshirikisha Diamond, ana zaidi ya mwezi sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa kujaa maji tumboni kulikosababishwa na tatizo la ini.

Kutokana na ugonjwa huo ameshalazwa katika hospitali ya Taifa ya muhimbili zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni ambao kuna wakati alikuwa akitolewa hadi lita nne.

Advertisement