Hawa ndo makocha wanaolipwa pochi nene Ligi Kuu England

LONDON, ENGLAND. MSIMU mpya wa Ligi Kuu England 2020-21 umeshaanza na kuna baadhi ya makocha wameshaonja utamu wa ushindi na wengine wameanza vibaya kwa vipigo kama ilivyo kwa Mreno, Jose Mourinho.

Jurgan Klopp ameingia uwanjani kwenye mchezo wa kwanza na kushinda 4-3 dhidi ya Leeds United, jambo linalofichua ugumu unaoweza kuwakabili Liverpool kwenye harakati zao za kutetea ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu.

Wakati mashabiki wengi wakifahamu mishahara wanayolipwa mastaa wanaokipiga kwenye ligi hiyo, ushaijiuliza kuhusu makocha, wanalipwa mshahara kiasi gani.

Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya makocha wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye Ligi Kuu England kwa msimu wa 2020-21.

Roy Hodgson - Pauni 93,750 kwa wiki

Maisha ya kocha mkongwe Roy Hodgson huko Crystal Palace si mabaya, ambapo mkataba wake wa kuinoa timu hiyo utafika tamati 2021, huku mshahara wake ukiwa Pauni 93,750 kwa wiki. Kwa hesabu hizo, Hodgson kwa mwaka mshahara wake ni Pauni 4.5 milioni. Kocha, Hodgson aliwahi kuinoa timu ya taifa ya England na Liverpool kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Brendan Rodgers - Pauni 105,000 kwa wiki

Kocha, Rodgers alionyesha uwezo mkubwa alipokuwa kwenye kikosi cha Swansea City na jambo hilo lilimfanya apate ajira kwenye klabu kubwa ya Liverpool, mahali ambako alikaribia kabisa kubeba ubingwa. Baadaye akaonyeshwa mlango wa kutokea na sasa anapiga kazi huko Leicester City, mahali ambako mshahara wake ni Pauni 105,000 kwa wiki huku mkataba wake ukifika mwisho 2025 na kwa mwaka analipwa Pauni 5 milioni.

Mikel Arteta - Pauni 105,000 kwa wiki

Kwenye msimu wake wa kwanza tu huko Arsenal, kocha Mikel Arteta alibeba mataji mawili, Kombe la FA na Ngao ya Jamii na huu ni msimu wake wa kwanza mzimamzima kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England. Kwa huduma yake anayotoa huko Emirates, Arteta analipwa mshahara wa Pauni 105,000 kwa wiki - sawa na Pauni 5 milioni kwa mwaka huku akiwa na mkataba utakaofika tamati 2023.

Ole Gunnar Solskjaer - Pauni 160,000 kwa wiki

Manchester United inasifika kwa kuwa moja ya klabu inayolipa mishahara mikubwa wachezaji wake. Jambo hilo halikuishia kwa wachezaji pekee, hata kocha Ole Gunnar Solskjaer naye analipwa vizuri, akipokea Pauni 160,000 kwa wiki kwenye mkataba wake utakaofika tamati 2022, ambao unamshuhudia kwa mwaka akiweka kibindoni mkwanja wa Pauni 7.8 milioni.

Marcelo Bielsa - Pauni 166,660 kwa wiki

Baada ya kuirudisha Leeds United kwenye Ligi Kuu England, kocha Marcelo Bielsa amekuwa na heshima kubwa kwenye kikosi hicho na hivyo kupewa dili tamu kabisa linalomfanya kwa wiki alipwe Pauni 166,000 sawa na Pauni 8 milioni kwa mwaka. Dili hilo la Marcelona huko Leeds United litafika tamati 2022, hivyo ataendelea kupiga mkwanja huo kwa miaka miwili zaidi.

Frank Lampard - Pauni 166,850 kwa wiki

Msimu wake wa kwanza kwenye kikosi cha Chelsea haukumaliza vibaya, ulimshuhudia Frank Lampard akiisaidia timu hiyo kumaliza kwenye nafasi ya nne katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England na hivyo kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Huduma bora imeandana na mshahara wake, ambapo Lampard analipwa Pauni 166,850 kwa wiki huku mkataba wake ukifika tamati 2022. Kwa mwaka analipwa Pauni 8 milioni.

Carlo Ancelotti - Pauni 230,000 kwa wiki

Mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu huu, Carlo Ancelotti amemwonyesha Jose Mourinho kwa nini yeye ni mkongwe baada ya kikosi chake cha Everton kwenda kuichapa Tottenham Hotspur ugenini. Mipango ya Ancelotti ni kuipa ubingwa Everton na dili lake alilosaini huko Goodison Park litakalomfanya kuwa hadi hadi 2024 linamfanya alipwe Pauni 230,000 kwa wiki - huku kwa mwaka akilipwa Pauni 11 milioni.

Jose Mourinho - Pauni 313,000 kwa wiki

Kocha Mreno, Jose Mourinho alisaini dili la miaka mitatu huko Tottenham Hotspur alipochukua mikoba Novemba 2019. Mkataba wake aliosaini huko Spurs utafika tamati 2023, huku ukimshuhudia akiwa analipwa Pauni 313,000 kwa wiki sawa na Pauni 15 milioni kwa mwaka. Jambo hilo linamfanya Mourinho kushika namba tatu kwenye orodha ya makocha wanaolipwa pesa ndefu zaidi kwenye Ligi Kuu England. Kwa mkataba wake wa miaka mitatu, Mourinho ataingiza hadi Pauni 50 milioni ukijumlisha bonasi.

Jurgen Klopp - Pauni 313,500 kwa wiki

Mjerumani, Jurgen Klopp ameisaidia Liverpool kumaliza ukame wa miaka 30 wa kubeba taji la Ligi Kuu England baada ya kubeba ubingwa msimu uliopita, wakati kikosi chake kilipokusanya pointi 99. Klopp alitua Liverpool mwaka 2015 na amepata mafanikio ya kutosha tu kwenye kikosi hicho ikiwamo kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akiliweka jina lake kwenye orodha ya makocha wanaolipwa mkwanja mrefu, Pauni 313,500 kwa wiki. Mkataba wake utafika tamati 2024. Kwa mwaka Pauni 15 milioni.

Pep Guardiola - Pauni 417,500 kwa wiki

Mhispaniao, Pep Guardiola kwa sasa ni kocha wa Manchester City na mara ya kwanza alipotua kwenye timu hiyo mwaka 2016 alisaini dili la miaka mitatu. Ndiye kocha anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England, ambapo kwa mwaka analipwa Pauni 20 milioni, ambazo ni Pauni 417,500 kwa wiki. Kabla ya kusaini mkataba mpya ambao utafika tamati 2021, Guardiola alikuwa akilipwa Pauni 14.6 milioni kwa mwaka, lakini baada ya kubeba mataji matatu ya ndani, mabosi wa Man City walimwongezea mkataba na kuboresha malipo yake, ambapo kwa wiki analipwa Pauni 417,500, ambapo kwenye kikosi cha Man City hakuna mchezaji anayelipwa pesa kiwango hicho.