Hawa mastaa wa England walivyojiachia kupiga bata

Friday February 14 2020

Hawa mastaa wa England walivyojiachia kupiga bata,LIGI Kuu England,Dubai na Maldives, Ligi Kuu England , Liverpool ,

 

LONDON, ENGLAND . LIGI Kuu England inarudi wikiendi hii baada ya siku kadhaa za mapumziko ambazo ziliwapata mastaa wanaokipiga kwenye mikikimikiki hiyo fursa ya kwenda kupumzisha akili na kula bata.

Michuano hiyo ya Ligi Kuu England iliingia kwenye mapumziko ya kupisha kipindi cha baridi, wakati makocha kadhaa kama Mikel Arteta na Ole Gunnar Solskjaer wakichukua vikosi vyao na kwenda kuweka kambi kwenye maeneo ya hali ya joto, baadhi ya wachezaji wao walitumia hilo kama nafasi ya kwenda kujipumzisha na kupiga bata kabla ya kurudi kuendelea na majukumu ya kumalizia msimu.

Klabu 12 kati ya 20 zinazomcheza kwenye ligi zilikuwa na mapumziko, hivyo wachezaji wake wanachukua nafasi hiyo kwenda kujivinjali kwenye viwanja mbalimbali hasa huko Dubai na Maldives.

Mastaa wa kikosi cha kwanza cha Liverpool waliruhusiwa kwenda kupumzisha akili licha ya kwamba walikuwa na mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Shrewsbury, ambapo wachezaji wa kikosi cha vijana walipewa jukumu la kucheza mechi hiyo.

Lakini mastaa wale wa kikosi cha kwanza waliruhusiwa na Kocha Jurgen Klopp kwenda kula bata kama walivyofanya Pierre-Emerick Aubameyang, Marcus Rashford na Fred kabla ya kwenda kujiunga na timu zao. Timu ya Aubameyang, Arsenal ilikuwa Dubai, wakati Rashford na Fred, timu yao Man United ilikuwa Marbella, Hispania.

Staa, Aubameyang alienda kula zake bata Abu Dhabi, wakati Rashford, ambaye kwa sasa ni majeruhi alikwenda kuponda raha Miami, Florida, ambako alionekana akipiga picha na Rapa Jay-Z.

Advertisement

Kiungo wa Man United, Fred alikwenda kula fungate lake la pili na mkewe huko Maldives, ambako alionekana tu akipiga mbizi tu kwa kujiachia.

Aubameyang aliwaonyesha mashabiki wake kwa kuwatuma picha kwenye Instagram akionekana kwenye ndege binafsi na ile ya kufurahia maisha huko Dubai akiwa na familia yake. Arsenal iliweka kambi yake ya mazoezi huko Falme za Kiarabu.

Kuhusu Rashford kwenye mtoko wake alipata pia fursa ya kwenda kushuhudia mechi ya Super Bowl XIV, wakati Fred alifurahia tu maisha yake na mkewe mrembo Monique Salum huko Maldives.

Lakini, mastaa wengi wa Ligi Kuu England walikwenda kula bata huko Mashariki ya Kati, ambako hali yake ya hewa kwa sasa ni joto. Fowadi wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi naye alikuwapo huko Dubai sambamba na staa wa Leicester City, James Maddison.

Staa wa Chelsea, Tammy Abraham aliungana na mchezaji mwenzake Fikayo Tomori kwenda kula bata ambapo walikutana na kutesa pamoja na mwimbaji wa Kinigeria, Davido huko Dubai.

Beki wa Man United, Diogo Dalot ni staa mwingine aliyekwenda kuponda raha kwenye jiji hilo la Falme za Kiarabu kama ilivyokuwa kwa kiungo wa Arsenal, Lucas Torreira kabla ya kuungana na wenzake kambini. Kipa wa Arsenal, Bernd Leno alikuwa na mpenzi wake mrembo Sophie Cristin huko huko Dubai kuponda raha.

Wachezaji wa kutoka timu za Wolves, Leicester City, Southampton, Burnley, Norwich, Liverpool, Aston Villa, Tottenham, Arsenal, Newcastle, Chelsea na Manchester United walikuwa na mapumziko kwenye wiki za kwanza na wikiendi hii watarejea kuendelea kwenye mechi, wakati klabu nyingine nane zilizobaki ikiwamo Manchester City zitakuwa na mapumziko na kwenye wiki hii na kurudi kuendelea na mchakamchaka wa ligi hapo baadaye.

Advertisement