Hawa hapa Man United walijiokotea tu

Muktasari:

Hata hivyo, historia pia inaonesha katika harakati hizi za usajili, Man United, inajivunia kufanya usajili wa wachezaji wazuri kwa bei ndogo na baadaye wakaibuka kuwa mastaa wakubwa. Hawa hapa ni baadhi ya nyota hao.

MASHETANI Wekundu, ni maarufu kwa kumwaga hela katika dirisha la usajili. Ubabe wao kwenye usajili, umewapatia wachezaji wazuri, lakini wakati mwengine wakiambulia kutumia fedha nyingi kusajili wachezaji, ambao mwisho wa siku hawarudishi fadhila.

Hata hivyo, historia pia inaonesha katika harakati hizi za usajili, Man United, inajivunia kufanya usajili wa wachezaji wazuri kwa bei ndogo na baadaye wakaibuka kuwa mastaa wakubwa. Hawa hapa ni baadhi ya nyota hao.

JAVIER HERNANDEZ

Kama United ingesema isubiri hadi baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2010, ingegharimika zaidi ya Pauni 6 milioni ilizokubali kutoa kwa ajili ya saini ya straika wa Mexico, Javier Hernandez’, kabla ya kuanza kwa fainali hizo, zilizofanyika Afrika Kusini.

Akiwa ndio ametoka kuifungia klabu yake ya Guadalajara mabao 21, Hernandez ‘Chicharito’, alikuwa mmoja kati ya nyota waliosumbua sana katika fainali hizo, akifunga mabao manne katika mechi nne= alizoichezea Mexico huko Bondeni.

Licha ya ukweli kwamba, Chicharito hakuwa straika namba moja katika kikosi cha Man United, bado alifanikiwa kufunga mabao 59, katika misimu minne aliyokaa Old Trafford, mara nyingi akiingia akitokea benchi. Alikuwa mwiba mchungu kwa Chelsea.

OLE GUNNAR SOLSKJAER

Unaweza kulipa Pauni 1.5 milioni kwa ajili ya saini ya straika, mwenye uwezo wa kufunga bao la ushindi kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Jibu ni ndio.

Vipi kuhusu hili, kutoa kiasi hicho cha fedha kwa straika anayefunga mabao 125 katika mechi 365, ambapo mechi 149 kati hizo aliingia akitokea benchi? Jibu linabaki kuwa ndio. Huyo ni kocha wa sasa wa Man United, Ole Gunnar Solskjaer, “the Baby-faced Assassin”.

PARK JI-SUNG

Licha ya kuteuliwa kuwania Tuzo ya Mshambuliaji Bora wa UEFA mwaka2005, akichuana na Ronaldinho, Andriy Shevchenko, Samuel Eto’o na Adriano, huwezi kuamini kuwa, Man United ilimsajili kwa Pauni 4 milioni tu, kutoka PSV.

“Alikuwa mchezaji mzuri sana, hasa katika mechi kubwa,” kocha wa zamani wa Man United, Alex Ferguson aliuambia mtandao wa klabu, ParkJi-Sung alipojiunga na QPR baada ya kuitumikia Man United kwa miaka saba:

“Nilikuwa napendelea sana kumchezesha katika mechi kubwa. Alikuwa na rekodi nzuri dhidi ya Arsenal. Kiwango alichoonesha dhidi ya Andrea Pirlo, huko Italia na Old Trafford, ni moja ya kumbukumbu nzuri alizoziacha katika akili ya mashabiki,” alisema Ferguson.

ERIC CANTONA

Hakuna kitu kizuri kama kumsajili mchezaji kutoka kwa hasimu wako kwa dau dogo la Pauni1.2 milioni. Inafurahisha zaidi, mchezaji huyo anapokuwa ni Mfaransa, Eric Daniel Pierre Cantona, halafu anakuja kuipatia klabu yako mafanikio makubwa ndani ya karne mbili.

EDWIN VAN DER SAR

Miaka sita baada ya kuondoka kwa Peter Schmeichel, hatimaye United ilimpata kipa mahiri aliyerithi nafasi yake langoni.

Huyu hakuwa mwengine, bali ni Mholanzi, Edwin van der Sar. Pamoja na kusajiliwa kwa Pauni 2 milioni tu, alikaa pale Old Trafford kwa miaka sita.

Katika miaka sita, Van Der Sar alikuwa chaguo la kwanza la United, akiisaidia kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya England (EPL) na ubingwa mmoja wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

NEMANJA VIDIC

“Unaweza ukashangaa kusikia alipotua Old Trafford akitokeaSpartak Moscow, kwa Pauni 7 milioni (2006), Mserbia Nemanja Vidic hakuwa na kiwango cha juu, kama alivyokuja kuwa baadae,” alisema Paul Scholes kumhusu Vidic.

Wakati anakuja United, Vidic alikuwa beki wa kawaida sana. Hakuwa na mabavu, alikuwa mwepesi sana. Hata hivyo, baada ya kujituma mazeozini, kila kitu kilibadilika. Hadi anaondoka Old Trafford (2014), alikuwa ni beki mahiri aliyehofiwa na kila mtu kwenye EPL.

TEDDY SHERINGHAM

Kutumia Pauni 3.5 milioni, kwa ajili ya mchezaji mwenye umri wa miaka31, haikuwa desturi ya Manchester United, katika usajili. Ujio wa nyota mwenye umri mkubwa kama huo, sio aina ya mchezaji ambaye mashabiki wa United, walitegemea angekuja kumrithi Cantona.

Hata hivyo, baada ya mwanzo mbaya wa maisha ya Old Trafford, hatimaye Teddy Sheringham, alifanya mambo makubwa. Hadi anafikisha miaka 35, Sheringham, alikuwa tayari ameshashinda tuzo ya PFA na FWA huku akitupia wavuni mabao 21.

PATRICE EVRA

Katika kupanga orodha hii, tulianza na wachezaji waliovaa jezi za Mashetani Wekundu, katika miaka ya hivi karibuni. Katika kupanga na kupangua, tukaangukia msimu wa 2005-06. Huu ni msimu ambao ulishuhudia ujio wa Edwin van der Sar, Park Ji-sung na Nemanja Vidic.

Msimu huo huo, United ilimsajili Mfaransa Patrice Evra, aliyesajiliwa Januari kwa Pauni 5 milioni akitokea Monaco. Beki huyu wakushoto, kama ilivyokuwa kwa Vidic, hakuanza vizuri, kabla kuibukakuwa mongoni mwa mabeki bora wa kushoto duniani.

CRISTIANO RONALDO

Uamuzi wa kutoa Pauni 12.24 milioni, kwa ajili ya kinda wa miaka 18,ambaye wala hakuwa na mafanikio yoyote, uliwaacha wengi mdomo wazi.

Lakini baada ya kutua Old Trafford na kufanya mambo aliyoyafanya, bila shaka Ronaldo alithibitisha ubora wake.

Miaka kadhaa baada ya kuisaidia United kutwaa mataji kibao, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ronaldo alitua Real Madrid, kwa Pauni milioni 80, huko akatwaa mataji mengine mengi, ikiwemo Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo.

Ronaldo mwaka jana amefanya uamuzi mgumu wa kuachana na Real Madrid na kutua Juventus kwa Pauni milioni 100. Mwaka huu ameiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa UEFA Nations League, Mwaka 2014 alitwaa taji la Euro, bila kusahau kuwa, ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara tano.