Havertz aviweka vigogo roho juu

Muktasari:

Havertz, ambaye saini yake imekuwa ikiwindwa na Chelsea, anajiandaa kukutana na mabosi wa klabu yake kujadili mustakabali wake klabuni hapo.

Munich, Ujerumani. Kocha wa Chelsea, Frank Lampard amesema bado ana uhakika wa kusajili mshambuliaji mwingine kwenye kikosi chake baada ya mfungaji wa RB Leipzig, Timo Werner.

Sasa huko Bayer Leverkusen kuna jambo wanataka kulifanya siku chache zijazo kuhusu mshambuliaji wao matata, Kai Havertz.

Havertz, ambaye saini yake imekuwa ikiwindwa na Chelsea, anajiandaa kukutana na mabosi wa klabu yake kujadili mustakabali wake klabuni hapo.

Juzi, Bayer Leverkusen ilipoteza mchezo muhimu wa fainali ya Kombe la Ujerumani mbele Bayern Munich kwa penalti 4-2. Imeshindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na mchezo huo ulikuwa karata yake ya mwisho.

Leverkusen ambayo imepamaliza nafasi ya tano kwenye Bundesliga, itacheza michuano ya Ligi ya Europa msimu ujao huku matamanio ya Havertz yakiwa kukipiga Ligi ya Mabingwa na Chelsea ambayo inasukwa upya kwa sasa, imeonyesha dhamira ya kutaka huduma yake.

Mbali na Chelsea, vigogo wengine wa Ulaya ikiwamo Bayern Munich, Real Madrid na Manchester United nazo zimekuwa zikimfuatilia kwa karibu Havertz msimu huu.

Tayari, Lampard amenasa huduma za Hakim Ziyech kutoka Ajax na Werner ambao wote wameigharimu pauni 81 milioni na sasa Chelsea inataka kuongeza mtambo mwingine wa mabao.