Hata Samatta huenda akasahulika kama De Mello

Friday January 11 2019

 

By SALIM SAID SALIM

WAPO waliochangia soka la Tanzania kwa aina ya kipekee, lakini kwa kutokuwepo kumbukumbu nzuri habari zao zimepotea hewani kama moshi wa kifuu.

Wakati wenzetu wanazo kumbukumbu za miaka mingi za mchezo huu sisi hatujalipa umuhimu suali hili. Si ajabu wachezaji mashuhuri wa sasa kama Mbwana Samatta wakawa hazijulikani habari zao miaka michache ijayo.

Sitashangaa kama wapo viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utapowatajia jina la Miraji wakakuuliza nani huyo?

Miraji aliyeishi Mtaa wa Rufita, Tabora mjini, alikuwa kipa mashuhuri wa Tanganyika kwa karibu miaka 10 na alitajika kama mlinda mlango bora Afrika ya Mashariki miaka ya 1950 hadi mwanzoni mwa 1960. Ukitembelea klabu kama Simba, Yanga au African Sports na Coastal Union za Tanga utakuta picha chache za wachezaji wa zamani na viongozi wachache ndio wanaojua majina yao na mchango walioutoa kwa klabu na nchi.

Nitazungumzia mchezaji aliyevuma nchini na baadaye Kenya ambaye sijazisikia miaka mingi habari zake kusimuliwa. Huyu ni Oscar de Mello.

Nilipokaa Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa 1965 hadi niliposema ‘Kwaheri Bongo’ 1985 mara nyingi na siku hizi nikiwa huko hutembelea baraza za kahawa.

Hapo soga hunoga wazee wakisimulia zama za ujana wao na hii imenisaidia kuchota mengi. Nimepata mengi sehemu hizi na kunisaidia katika uandishi wa michezo, lakini siku moja nilipigwa na butwaa katika baraza moja pale Rozana, Buguruni, mzee mmoja alipozungumzia zama za ujana wake miaka ya 1960. Alidai Waswahili tu ndio waliofika Uwanja wa Mzizima (Ilala), sasa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, kuangalia kandanda na hawakuchezea klabu za Waswahili.

Sikuongeza langu kwa kuchelea kuchafua baraza. Nilitulia kimya kama kuku aliyekuwa anataga.

Nimeona vizuri nieleze hali ya michezo ilivyokuwa Tanganyika zama za ukoloni, tafauti na majirani zetu. Walikuwepo watu ambao sio Waswahili waliochezea klabu za mitaani, zikiwemo Sunderland (Simba) na Yanga na wengine walisaidia vifaa na fedha na walikuwa viongozi.

Wapo waliozuiliwa kuichezea Tanganyika katika Kombe la Gossage, (siku hizi Kombe la Challenge). Sheria ya Gossage ilieleza mashindano yale yalikuwa ni kwa Waafrika, Waarabu na Wahindi tu, lakini haikutumika kwa michezo mengine ya kimataifa.

Magoa (watu wa Goa, India), hata waliozaliwa Tanganyika, hawakuruhusiwa kucheza Kombe la Gossage kwa vile walihesabika ni Wazungu.

Sijui sheria ile ilikuwa na maana gani, labda kwa vile Magoa walizungumza zaidi Kiingereza kuliko Kiswahili.

Ukiangalia picha za zamani ziliopigwa katika Uwanja wa Mzizima, hasa ilipofanyika michezo mikubwa utaona watazamaji walikuwa wa kabila zote, wakiwemo Wazungu.

Miongoni mwa watu waliokuwa hawakosi kufika uwanjani hasa Tanganyika ilipocheza ni gavana wa mwisho, Sir Richard Turnbull ambaye wapo wachezaji aliowapenda sana.

Kila ililipocheza timu ya Tanganyika, Gavana alipeleka ndege Songea kumchukua na kumrudisha mchezaji mahiri Edward Akwitende aliyekuwepo huko akifanya kazi katika Jeshi la Polisi.

Gavana alisema timu ya Tanganyika ilikuwa haikamili bila ya Akwitende uwanjani.

Miongoni mwa wachezaji mashuhuri wa zama hizo aliyeng’ara na timu za mitaani na kuiwakilisha Tanganyika na baadaye Kenya katika michezo ya kimataifa (sio Kombe la Gossage) ni huyu Oscar de Mello. Wazazi wake ni wa asili ya Goa, India, lakini alizaliwa Dar es Salaam 1930. Baadaye alihamia Kenya na nilipokutana naye mara alinielezea maisha yake ya kupigana vikumbo na Waswahili wa Jangwani, Kariakoo na Gerezani. Baada ya kucheza mitaaani alijiunga na Dar Wanderers (sio hii iliyopo Temeke hivi sasa). Katika mwaka 1950 alijiunga na Dar es Salaam Sunderland na kuwa mtu wa kwanza ambaye si Mwafrika kuichezea klabu hii japo ilikuwa na mashabiki wa makabila mbalimbali.

Alikaa na Sundreland na kuwa miongoni mwa wachezaji nyota hadi 1956 ambapo rafiki yake Peter Tino (sio huyu mchezaji wa zamani wa Taifa Stars) alipomchukua Nairobi kufanya kazi na kampuni iliyokuwa wakala wa kiwanda cha Tanganyika Packers kiliopo Kawe, Dar es Salaam.

Huko alichezea timu za Kenya na timu ya taifa na kuwa mwamuzi ambaye mara nyingi alishambuliwa alipowachezesha mahasimu, Abaluhya (sasa Leopards) na Luo Union (sasa Gor Mahia).

Siku moja katika mwaka 1967 nikiwa na waamuzi Dustan Daffa na Carneiro (Goa) aliyekuwa Katibu wa Chama cha Soka cha Tanganyika, Kitwana Ibrahim, alielezea ushupavu wa De Melllo alipokuwa mlinda mlango.

Hii ilitokana na mjadala wa mchezo uliofanyika Ilala ambapo Carneiro alikuwa mwamuzi. Carneiro alilikataa goli baada ya mpira uliopigwa kichwa ulipokuwa unalekea nje ya uwanja kumgonga yeye (Carneiro) kichwa alipokuwa pembezoni mwa mlingoti wa goli na kuingia kimiani.

Kitwana alimwambia Carneiro:” Magoa ni watu wa ajabu kwa kupiga vichwa. Alikuwepo Goa mwenzako, De Mello wa Sunderland ambaye siku moja aliokoa penalti kwa kuupiga kichwa”. Alimwambia Carneiro tumeona Goa mwengine akiwa mwamuzi anaisaidia timu kupata bao la kichwa.

“Nadhani tokea sasa ukichezesha mpira ni vizuri ukatuambia wewe ni mchezaji wa 12 wa timu ipi”, Kitwana alisema. Tulicheka, lakini kwangu huo ulikuwa ushuhuda wa umahiri wa Mello, kipa wa zamani wa Sunderland.

Katika mwaka 1973 De Mello alichaguliwa Mshika Fedha wa Chama cha Soka cha Kenya na kuiwakilisha Kenya katika mikutano ya Shirikisho la Kimataifa la Duniani (Fifa).

Watoto wawili wa kike, Louisa na Valerie, waling’ara kama wachezaji wa tennis na kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya Afrika Mashariki na nje kabla ya kuhamia Canada. De Mello alibakia Kenya na kuwa na maisha ya kimya baada ya mama watoto wake, Zelia, kufariki katika ajali ya gari alipotoka kuchezea tenisi na kuelekea nyumbani nyakati za jioni.

Lakini mara nyingi alifika viwanjani kuangalia soka na kusalimiana wachezaji wa zamani wa Abaluhya na Luo Union. Oscar de Mello alifariki na kuzikwa Nairobi mwaka 2008. Nimemzungumzia De Mello ili kutadharisha jamii na waandishi wa habari nchini juu ya athari na hatari za kupotosha historia. Hii ni kwa sababu ukibuni jambo litalozusha hisia za chuki ni sawa na kukaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno kutafuna. De Mello anafaa kukumbukwa katika historia yetu ya soka kama mmoja wa wachezaji wazuri wa timu ya Tanganyika

Advertisement