Hassan Kessy nyavu sasa zinamtambua

Muktasari:

  • Huu ni msimu wa pili kwa Kessy (25) ambaye ni mzaliwa wa Morogoro akiwa na Nkana ambayo alijiunga nayo Agosti 3 mwaka jana akitokea Yanga.

BAADA ya kuondolewa kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na CS Sfaxien ya Tunisia, Nkana anayoichezea beki wa Kitanzania, Hassan Kessy imehamishia hasira zao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Zambia dhidi ya Power Dynamos.

Chama la Kessy limetoa dozi ya mabao 2-0 ugenini kwenye mchezo ambao alishuhudiwa mchezaji huyo wa zamani wa Yanga akipachika bao lake la kwanza msimu huu wa 2018/19.

Kessy alifunga bao hilo kipindi cha pili huku bao lao la kwanza likipatikana kipindi cha kwanza kupitia kwa Ronald Kampamba.

Nkana iliondolewa dhidi ya CS Sfaxien, Aprili 14 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2 kutokana na kupoteza mchezo wa marudiano kwa mabao 2-0. Mchezo wa kwanza Zambia, Aprili 7 walishinda kwa mabao 2-1.

Huu ni msimu wa pili kwa Kessy (25) ambaye ni mzaliwa wa Morogoro akiwa na Nkana ambayo alijiunga nayo Agosti 3 mwaka jana akitokea Yanga.

Kabla ya kutua Yanga, Kessy alikuwa beki wa Simba na uhamisho wake kutua Jangwani ulizua mvutano kati ya miamba hao wawili nchini.