Harambee Stars, Taifa Stars, patachimbika

Muktasari:

Timu hizo zinafanana katika rekodi mbalimbali za mechi, washambuliaji Stars hatari zaidi vipindi vyote

Dar es Salaam. Leo, majira ya saa tano usiku, Taifa Stars ya Tanzania itavaana na Harambee Stars ya Kenya katika mchezo unaotabiriwa kuwa mkali kati ya majirani hao wa Afrika Mashariki.

Mechi hiyo ni mwendelezo wa michezo ya Kundi C kwenye michuano ya AFCON inayoendelea kupigwa jijini Cairo, Misri.

Timu hizo zinaingia katika Uwanja wa June 30, huku kila moja ikiwa na kumbukumbu mbaya ya mechi ya kwanza. Katika mechi ya kwanza Kenya ilikutana na Algeria na kuambulia kichapo cha mabao 2-0 yaliyofungwa na Baghdad Bounedjah (dakika 34, penalti) na Riyad Mahrez (dakika ya 43).

Nayo Tanzania ilikuwa na matokeo kama hayo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Senegal yaliyofungwa na Keita Balde Diao (dakika ya 28) na Krepin Diatta (dakika ya 64).

Matokeo hayo ya kujeruhiwa yanaonyesha kwamba kila timu ina njaa ya kupata pointi na ni wazi kwamba katika mchezo wa leo ni lazima patachimbika.

Tanzania chini ya kocha Emmanuel Amunike imejizatiti kuhakikisha kuwa inashinda huku jukumu kubwa likiwa kwa nyota Mbwana Samatta, anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji.

Kwa upande wa Kenya watakuwa wakimtegemea mpachika mabao Michael Olunga ambaye anacheza katika Ligi Kuu ya Japan.

Kocha Amunike amesema kila kitu kiko sawa na anataka kuhakikisha wanapata ushindi.

Kwa upande wa kocha wa Kenya, Sebastien Magne ameitaja kuwa ni mechi muhimu watakayohakikisha wanapata ushindi ili wasonge mbele.

Ni wazi kwamba timu hizo zina presha kubwa hasa kwa kuangalia rekodi ya mechi zao 10 za karibuni.

Katika rekodi ya mechi 10 za mwisho ambazo kila timu imecheza inaonekana kushabihiana jambo linaloashiria kuwa mechi hiyo ni ngumu kutabirika.

Rekodi hizo zinaonyesha kuwa kasi ya washambuliaji wa Kenya na Stars katika kufumania nyavu na ufanisi wa safu za ulinzi katika kulinda lango unaelekea kufanana.

Katika michezo 10 ya mwisho washambuliaji wa Kenya wamefunga mabao 11 sawa na Stars, huku mabeki wa timu hizo wakiachia mabao saba kila moja achilia mbali yale waliyofungwa juzi kwenye mechi za AFCON.

Katika mechi 10 za mwisho Kenya imeshinda mara tano, imetoka sare mbili na kufungwa michezo mitatu dhidi ya India 3-0, India 2-0 na Ghana 1-0.

Imeshinda 4-0 dhidi ya China, 1-0 na Ghana, 1-0 na Malawi, 3-0 na Ethiopia na bao 1-0 dhidi ya Madagascar huku ikitoka sare ya 1-1 na DR Congo na suluhu dhidi ya Ethiopia. Stars imeshinda mara nne, imefungwa mara tatu na kupata sare tatu ya bao 1-1 dhidi ya Zimbabwe, matokeo kama hayo dhidi ya Benin na suluhu na Uganda.

Vievile imeshinda 2-0 dhidi ya Cape Verde, 3-0 na Uganda, 2-0 na DR Congo na matokeo kama hayo dhidi ya Malawi huku ikifungwa 3-0 na Cape Verde, 1-0 na Lesotho na matokeo kama hayo dhidi ya Misri.

Dakika za hatari

Wakati rekodi zinaonyesha washambuliaji wa Stars chini ya Nahodha Mbwana Samatta wana uwezo wa kupachika mabao katika vipindi vyote viwili, beki ya Stars yenyewe katika michezo mitatu kati ya 10 wamefungwa zaidi kipindi cha pili ambapo waliruhusu mabao matatu dakika za 64, 76 na 85 na mawili katika dakika za 16 na 23.

Kenya inayoongozwa na kiungo mshambuliaji Victor Wanyama anayecheza Tottenham Hotspurs katika mechi 10 za mwisho, mabeki wake wamefungwa mabao mengi kipindi cha pili ambapo katika saba waliyofungwa kwenye mechi hizo, matano yamefungwa kipindi cha pili dakika 68, 90+1, 71, 82 na 87 wakati mawili yamefungwa kipindi cha kwanza katika dakika za nane na 29.

Washambuliaji wa timu hiyo ni hatari zaidi pia kipindi cha pili ambapo katika mabao 11 waliyofunga kwenye michezo 10, saba wamefungwa kipindi cha pili na manne cha kwanza huku matatu yakiwa ya penati ambapo mawili yalifungwa na Wanyama kipindi cha pili.

Katika mabao 11 ambayo Kenya imefunga kwenye michezo 10 ya mwisho, saba yamefungwa dakika za 52, 54, 89, 69, 78, 67 na 64 ilhali manne yamefungwa dakika za 40, 23, 27 na 25.

Katika hatua nyingine, nyota wa Taifa Stars, Samatta alisema mechi hiyo itakuwa ngumu lakini watahakikisha wanapambana kupata pointi ambazo zitawaweka katika nafasi nzuri.