Panachimbika Ligi Daraja la Kwanza leo

Saturday January 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

KIVUMBI cha Ligi Daraja la Kwanza kinaendelea leo Jumamosi ambapo  nyasi za viwanja nane zitawaka moto, lakini TFF imetoa onyo kali kwa wale wataalamu wa kupanga matokeo wakijaribu, wataadhibiwa.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema, haitavumilia kitendo chochote kitakachojihusisha na hujuma ya upangaji wa matokea na watawachukulia hatua kali wale wote watakaojihusisha na matukio hayo.
Waamuzi watakaochezesha mechi hizo wametakiwa wajikite katika kuchezesha kwa haki na Tff imeviandikia barua vyombo vyote vya ulinzi na usalama kufuatilia hatua hizo za michezo ya mwisho.
Katika michezo hiyo ya kundi A,  Uwanja wa Filbert Bayi kutakuwa na mchezo kati ya Kiluvya United dhidi ya Mgambo JKT wakati  Mvuvumwa watacheza na JKT Ruvu Uwanja wa  Uhuru jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine ni za kundi B, Coastal Union itaikaribisha Mufindi United  kwenye Uwanja wa Mkwakwani,  JKT Mlale itacheza na Mawenzi Market  Uwanja wa Majimaji na Mbeya Kwanza itakipiga dhidi ya KMC Uwanja wa Sokoine.
Katika michezo ya kundi C, Toto Africans itacheza na JKT Oljoro, Rhino Rangers na Dodoma FC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na Biashara United itacheza n Alliance School.