Hao Barca wanapiga pesa nje, ndani

Muktasari:

  • Najongea na mashabiki na rafiki yangu Scoba. Nafika uwanjani mapema kudadisi. Unakutana na mambo mawili makubwa. Kwanza kabisa ni maduka machache madogo yalipo nje ya uwanja kuzuguka uwanja mzima.

KWA kutumia treni au wenyewe wanaita Metro naelekea Uwanja wa Barcelona, Camp Nou. Unashuka katika kituo cha treni kinachoitwa Colliblanc.

Unaweza kushuka Kituo cha Badal pia na bado ukaungana kwa mbele na wale walioshuka katika Kituo cha Collblank kwa ajili ya kuanzisha maandamano ya kwenda uwanjani.

Maandamano? Ndio. Ni neno sahihi kwa sababu ndani ya treni wamejaa watu wengi wanaokwenda uwanjani. Lakini zaidi ni kwamba mnaposhuka mnajikuta katika msafara wa kutembea kwa pamoja kwa mwendo wa nusu kilomita kwenda uwanjani.

Camp Nou maana yake halisi ni ‘Kambi Mpya’. kwa Kihispaniola Nou ni New, au Mpya. Ni uwanja ambao umejengwa mjini.

Umezungukwa na mji. Mnapotembea kwenda uwanjani mnapita katika maduka kama vile mtaa wa Samora. Lakini zaidi mnapita katika pub mbalimbali na watu wanakunywa bia nje na ndani ya pub hizo. Hawana haraka. Utaratibu wa kuingia ni mzuri.

Najongea na mashabiki na rafiki yangu Scoba. Nafika uwanjani mapema kudadisi. Unakutana na mambo mawili makubwa. Kwanza kabisa ni maduka machache madogo yalipo nje ya uwanja kuzuguka uwanja mzima.

Yanauza jezi na vifaa mbalimbali vya rangi ya Barcelona. Kama nilivyosema jana. Jina lililoambatana zaidi katika jezi na vifaa hivyo ni Lionel Messi 10.

Kando ya uwanja kuna duka lao kubwa. Duka rasmi la klabu. Ingawa naambiwa kwamba hata maeneo mengine mjini kuna maduka makubwa ya klabu. Hapo unakutana na wageni mbalimbali wakinunua jezi na fulana. Hili ni duka kubwa ambalo lina eneo katikati, juu na chini. Huku juu unapanda na ngazi, kule chini unashuka na ngazi.

Watu ni wengi lakini nahisi nusu ya watu waliopo dukani inawezekana ni watalii waliotoka nje ya Jiji la Barcelona au nje ya Hispania kama mimi. Wengi wananunua jezi ya Messi. Nakutana na raia wawili wa Wakenya wapenzi wanaoishi London, tunapiga stori kidogo, kisha kila mtu anaendelea na hamsini zake.

Duka hili la Barcelona ni la kisasa zaidi. Lina picha za mastaa wao, TV kubwa zinazoelezea historia yao. Hapo pia unakumbushwa video za mastaa wao wa zamani akina Patrick Kluivert, Rivaldo, Carles Puyol na wengineo. Wenzetu wanajua jinsi ya kuendelea kuwaenzi mastaa wao.

Kwa pesa ya madafu ya Tanzania ni wazi kwamba jezi zao pamoja na fulana zao ni ghali. Zinaanzia Euro 70 na kuendelea. Zaidi ya Sh 140,000 kwa moja. Unapoishi au kutembelea Ulaya usipende sana kuitafsiri pesa yetu kwa yao. Hautanunua kitu.

Hatimaye Barcelona wanafanikiwa kuchukua zaidi ya sh 200,000 zangu za Kitanzania kwa kununua fulana mbili tu. Sijutii. Mwanadamu anaishi mara moja.

Unaendelea kugundua ni kwa namna gani klabu inaingiza pesa nyingi kupitia mauzo ya jezi na vifaa vingine. Hii ni achilia mbali viingilio vingine na vyanzo vingine vya mapato.

Nje ya Uwanja wa Nou Camp kuna sehemu za kuuzia tiketi za aina mbili. Za kwenda uwanjani na zile za kwenda kuzunguka kutalii ndani ya uwanja katika siku ambazo sio za mechi. Unazungushwa uwanjani kwa ajili ya kwenda kutazama mambo mbalimbali na historia ya klabu yao.

Mtu mmoja anawazungusha kuwaonyesha vyumba vya kubadilishia nguo vya wachezaji wa Barcelona na timu ya ugenini. Unaonyeshwa wapi ambapo Messi huwa anakaa wakati anabadilisha jezi zake. Mabafu yao, vyoo vyao, na kila kitu. Mnaonyeshwa sehemu ya kuchezea (pitch) kwa karibu.

Mnaonyeshwa picha za mastaa wa zamani, makombe, na mambo mengine. Hayo yanaendelea huku watu wakipiga picha za ukumbusho. Huduma hii inalipiwa kwa Euro 30 (Sh 70,000)

Klabu inapiga pesa kiulaini hata kama hawachezi. Hata kama wachezaji wameondoka kurudi makwao kwa likizo kama ilivyo sasa.

Fahama hata dakika hii unayosoma hii makala Barcelona wanaingia pesa kupitia uwanja wao wa Camp Nou kwa njia halali kabisa. Klabu zetu zimelala.

Itaendelea Alhamisi