Hanspope aunganishwa kesi Aveva, Kaburu

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe ameunganishwa katika kesi inayowakabili waliokuwa viongozi wa klabu hiyo Evans Aveva na Geofrey Nyange ‘Kaburu’.

Hanspope anakabiliwa na mashtaka mawili kati ya 10 yanayowakabili vigogo hao wa Klabu ya Simba ambayo ni kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Dar es Salaam. Hatimaye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zakaria Hanspope amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka mawili ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Hanspoppe ambaye ni mmoja wa washtakiwa katika kesi inayowakabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliyekuwa akitafutwa na Mahakama.

Hanspope alipandishwa kizimbani mahakamani jana Oktoba 16, 2018 na kuunganishwa na washtakiwa Aveva,  Nyange na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Kutokana na kuunganishwa katika kesi hiyo, upande wa mashtaka umelazimika kuwasomea mashtaka upya washtakiwa wote watatu.

Kati ya mashtaka 10 yanayowakabili washtakiwa wote wanne katika kesi hiyo akiwemo mfanyabiashara Frank Lauwo ambaye bado hajafikishwa mahakamani hapo, Hanspope anakabiliwa namshtaka mawili.

Akimsomea mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Thomas Simba,  kuwa Hanspope anakabiliwa na mashtaka mawili kati ya 10 yanayowakabili vigogo hao wa Klabu ya Simba.

Mashtaka hayo ni pamoja na shtaka la kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

katika shtaka la kwanza, inadaiwa Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama na kutenda kosa ya matumizi mabaya ya Ofisi na tukio hilo wanadaiwa kulitenda Mei 30, 2016 Dar es Salaam kwa nia ya kughushi hati ya malipo ya Mei 28,2016 kuonyesha kuwa Klabu ya Simba ilinunua nyasi bandia za thamani ya Dola za Marekani 40,577, wakati wakijua kuwa siyo kweli.

Katika shtaka la pili ambalo ni matumizi mabaya ya Ofisi kwa kuandaa nyaraka ya kuomba kuhamisha fedha linalomhusisha Hanspope,

Pia, wakili Kimaro amesema katika shtaka la tisa,  washtakiwa wote kati ya Machi 10 na Mei 30, 2016, waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha kuwa Klabu ya Simba ilinunua nyasi bandia kwa thamani ya Dola za Marekani 40,577, wakati wakijua ni uongo kinyume cha Sheria ya Kodi ya Mapato.

Hanspope amekana mashtaka na wakili wake, Augustine Shio alimuombea dhamana mteja wake akidai mashtaka dhidi yake yanadhaminika.

Hakimu Simba alitaja masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambulika kisheria,  watakaotia saini saini bondi ya Sh15milioni kila mmoja.

Hanspope alitimiza masharti ya dhamana na ameachiwa huru kwa dhamana.

kesi hiyo imeahirishwa hadi,  Oktoba 19,mwaka huu ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali (PH).

Wakati huo huo, kesi inayomkabili, aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi na wenzake wanne imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo ilipaswa kuendelea kusikilizwa jana Oktoba 16, 2018 , mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri lakini wakili anayesimamia shauri hilo  Leonard Swai, amesafiri na yupo nje ya Dar es Salaam.