HISIA ZANGU: Rweyemamu atakuwa mtu wa mwisho kuihujumu Simba

NASIKIA mtu anayeitwa Patrick Rweyemamu naye ameondolewa katika nafasi ya Umeneja wa Simba. kisa? Zinatolewa sababu nyingi. Lakini nadhani matokeo ya karibuni ya Simba yamewachanganya viongozi.

Walifungwa 1-0 na Tanzania Prison pale Sumbawanga. Wakafungwa 1-0 na Ruvu Shooting ya Masau Bwire. Simba ikaibuka na uamuzi mazito. Zinaweza kutolewa sababu nyingine kufukuzwa kwa mtu kama Rweyemamu.

Zinaweza kuja sababu nyingine za Kidiplomasia zaidi kama vile ‘kubana bajeti’, . inawezeka kuja sababu nyingine kama vile ‘amepatikana mtu bora zaidi’. Zinaweza kuja sababu nyingi. Unajiuliza, kwanini uamuzi umechukuliwa baada ya Simba kupoteza mechi mbili mfululizo?

Baada ya hapo zinakuja tetesi za hujuma. Hizi ndizo zimezagaa zaidi. Kwamba anahusika kuihujumu Simba. Hapo ndipo ninapopata shida zaidi. Ili iweje? Ili apate nini zaidi? Ili Yanga awe bingwa? Ili Azam awe bingwa?

Mtu mmoja mzito wa ndani ya timu akaniambia Patrick na aliyekuwa kiongozi wa Simba, Hashim Mbaga wote wapo katika mkumbo mmoja wa kuihujumu Simba. Simfahamu vizuri Mbaga lakini namfahamu Patrick. Aihujumu Simba ili iweje?

Sina mawasiliano ya karibu na Patrick katika siku za karibuni lakini namkumbuka kwa moyo wake wa zamani wa kuisadia Simba katika nyakati ngumu. Wakati ule ambapo alikuwa anahangaika na soka la vijana wakati nchi ikiwa imezama katika soka la wakongwe.

Pale Simba walikuwa wameunda timu imara ya vijana huku wakongwe wao wakiendelea kucheza. Ni hawa akina Ibrahim Ajib, Abdala Seseme, Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Gallas na wengineo wengi. Huyu Patrick ndiye ambaye alikuwa anaburuzana nao kuanzia majumbani mwao.

Wakati fulani aliwahi kunisimulia jinsi ambavyo alikuwa analazimika kushinda nyumbani kwa Ajib kwa ajili ya kumshawishi aende akafanye mazoezi Simba ya vijana. Bila ya kumpitia Ajib basi Ajib alikuwa haendi mazoezini. mvivu. Kazi ya Patrick ikawa kumpitia nyumbani.

Maisha ya Patrick pale Simba yalitawaliwa na soka na la vijana ingawa kwa kiasi kikubwa alikuwa akishiriki pia katika timu ya wakubwa. Wakati fulani alishinda mtaani kwetu kwa ajili ya kumshawishi kiungo wa Mtibwa, Shaban Nditi asaini Simba.

Wakati ule Nditi alikuwa amechomoza Mtibwa na Simba ilikuwa inawasaka Nditi na kiungo mwingine wa Mtibwa, Nico Nyagawa. Nditi alikuwa anasita kwenda Simba kwa hofu ya kucheza nafasi moja na Suleiman Matola.

Huyu Patrick alikuwa anashinda nyumbani kwa akina Nditi siku nzima huku Nditi akiwa amejificha hajulikani alipo. Mwishowe walifanikiwa kuinasa saini yake ingawa mambo hayakwenda poa kwa Nditi pale Msimbazi.

Kituko kikubwa ambacho Patrick aliwahi kunisimulia zamani ni namna alivyohatarisha maisha ya ndoa yake. ilikuwa ni baada ya kuuza gari la Mkewe kwa ajili ya kupata pesa za kuisaidia Simba. wakati mwingine watu wa Simba na Yanga wanafanya mambo ya ajabu kwa ajili ya timu hizi. Ndio maana hazifi.

Leo tunaishi katika dunia ya hujuma. Timu zetu kubwa zikifungwa linakuja neno hujuma. Wanashtumiana wenyewe kwa wenyewe ndani ya klabu lakini pia huwa wanawashutumu wapinzani wao wa karibu. Ni kama ambavyo, Mwinyi Zahera alipokuwa akidai Simba ilikuwa inawahujumu hata pale ambapo washambuliaji wake akina, Yikpe walipokuwa wakikosa mabao ya wazi katika mechi zao.

Mdudu aliyepo Simba ni kwamba kuna hujuma za ndani kwa ndani. Labda kuna watu wanashirikiana na watu wa Yanga kuihujumu timu. Hapo ndipo ninapojiuliza inawezekana vipi mtu kama Patrick akaihujumu timu ambayo ameitumikia kwa machozi, jasho na damu.

Na huwa najiuliza kuhusu jukumu la Meneja. Ni lipi hasa? Kuhakikisha timu ipo salama kambini. Kukusanya pasipoti kwa ajili ya safari. Kuandaa utaratibu wa kwenda mazoezini. Na mengineyo. Kiufundi hauoni ni wapi anaweza kuhujumu timu.

Niliwahi kuambiwa Patrick alikuwa pale kwa sababu ya baadhi ya viongozi ambao walikuwa wanataka awaunganishe vema na kocha wao mtata wa kizungu. Labda alikuwa haivi na viongozi wengine ndio maana wamemtimua.

Ukweli ni kwamba sioni mambo mawili kwa uwazi. Yeye kuihujumu Simba au yeye kuhusika na vipigo vya Simba moja kwa moja. Huku kwa sababu za kiufundi kuna suala la kocha au wachezaji au waamuzi wa mechi,

Pambano dhidi ya Prison Simba ilinyimwa penalti mbili na mwamuzi, Shomari Lawi. Pambano dhidi ya Ruvu wakajikuta wakikosa penalti kupitia kwa nahodha wao, John Bocco. Lakini hapo hapo ikumbukwe Simba ilipoteza nafasi kadhaa za wazi ambazo ni sehemu ya mchezo na ambazo wamekuwa wakizipoteza hata katika mechi wanazoshinda. Kama Lawi angetoa zile penalti, kama Bocco na wenzake wangetumia nafasi vizuri mechi ya Ruvu si ajabu leo lugha ya hujuma isingekuwepo. Tatizo labda kama kumekuwa na kuviziana ndani ya kambi yao wenyewe.

K a haraka haraka ni ninachokiona katika matokeo ya Simba ni timu pinzani kuikamia zaidi Simba huku waamuzi wakishindwa kufanya kazi zao vema, mfano ni Lawi. Simba imekuwa ikitangaziwa vita na klabu nyingi ambazo wanacheza nazo.

Wapinzani wao wamekuwa wakicheza rafu na kufanyiana ubabe mwingi na wachezaji wa Simba. Waamuzi wamekuwa wapole kidogo katika jambo hili. Wachezaji wa Simba hawaonekani kuwa tayari kwa upinzani huu.

Kuna hisia zinatambaa kwamba Simba ukiwachezea ubabe huwa wananywea. Sitaki kuamini hisia hizi kwa urahisi. Simba nao wao tayari kwa lolote uwanjani. Mara nyingi maisha hayawi rahisi baada ya timu kutwaa mataji matatu mfululizo.