HISIA ZANGU: HII HAPA NI HATIMA YA SAMATTA ASTON VILLA

TUNA staa mmoja tu wa ukweli katika soka letu nje ya mipaka yetu. Mbwana Samatta ‘Poppa’. Juzi ilipokuja taarifa kwamba Aston Villa wana mpango kumtia sokoni ilinyong’onyesha mashabiki kwa kiasi kikubwa.

Mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu ya England. Anawezaje kucheza kwa miezi nane tu kisha auzwe na kwenda kwingineko? Tuna bahati mbaya kiasi gani? Haiwezekani.

Mtazamo wangu baada ya kupata taarifa hizi ni huu hapa. Waandishi wengi wa habari wa Kiingereza huwa wanapenda kumchomoa mchezaji mmoja pindi mchezaji mwingine anapokuja. Ujio wa staa mpya, Ollie Watkins kutoka Brentford ulikuwa unamaanisha kwamba waandishi wa Kiingereza wangejaribu kumchomoa staa mmoja kwa ajili ya kupisha ujio wake.

Pale Aston Villa kabla ya Ollie kulikuwa na washambuliaji watatu. Samatta, Mbrazil Wesley pamoja na mtoto wa Kiingereza, Keinan Davis. Kwa mtazamo wa waandishi wa Kiingereza ni kwamba mshambuliaji mmoja lazima apishe ujio wa Ollie.

Nadhani kwao wameona kuwa mshambuliaji huyu ni Samatta. Kwanini? Labda kwa sababu Wesley ni Mbrazil na hawajaona sababu ya kuondoka kwake kwa sababu ya ukubwa wa Taifa lake. Davis? Labda kwa sababu ni mtoto wa Kiingereza. Tunajua jinsi Waingereza wanavyopenda watu wao.

Mhanga wao amekuwa Samatta. Ni Mtanzania. Taifa dogo katika soka. Lakini tuangalie. Nani zaidi kati ya Davis na Samatta? Kwangu mimi ni Samatta. Rekodi zake za mabao za alikotoka zipo wazi. Lakini tangu atue Aston Villa amefunga mabao mawili.

Tangu Samatta atue Villa hatujamuona Davis akifunga. Amekuwa akitumia nguvu zaidi na anasifiwa kwamba anatawala mabeki kuliko Samatta. Hata hivyo katika shida kama ambayo Villa walikabiliana nayo msimu uliopita nadhani washambuliaji wao waliangaliwa zaidi katika suala la ufungaji. Davis hakuwa na maajabu katika ufungaji.

Unapojaribu kumlaumu Samatta peke yake kwamba hakufanya maajabu tunapaswa kujiuliza, wakati Samatta alipokuwa anaanzia nje na Davis kuanza, huyu Davis alikuwa na maajabu gani? Na hata kabla ya hapo ana rekodi zipi za ufungaji?

Huyu Wesley mwenyewe alikuwa Ligi moja na Samatta pale Ubelgiji. Wakati Samatta akiibuka kuwa mfungaji bora pale Ubelgiji akifunga mabao 23, huyu Wesley alikuwa anachezea Gent na alifunga mabao 14 tu.

Kilichompeleka Villa haraka ni Ubrazil wake, lakini pia ana umbo kubwa ambalo linaonekana kufaa kwa Ligi Kuu ya England. Hii ni faida ambayo kwa soka la Kiingereza ilimchelewesha Samatta Ubelgiji lakini angeweza kuja England mapema zaidi.

Ni wazi kwamba Samatta angekuwa ni Mnigeria au Mcameroon angeweza kutua England mapema zaidi kutokana na rekodi zake nzuri za upachikaji wa mabao. Wote tunafahamu hili na tumelizungumzia kwa muda mrefu.

Naamini Samatta atabakia Villa. Msimu unaoweza kuamua hatima ya Samatta ni huu hapa ulioanza juzi. Samatta alihitaji kuzoea Ligi Kuu ya England na zaidi alihitaji kuwa na maandalizi kamili ya mwanzo wa msimu (Pre Season) kwa sababu kumbuka kwamba alihamia Januari.

Wachezaji au makocha huwa wanahukumiwa zaidi na Pre Season. Hata kwa makocha, ingekuwa ngumu kwa Arsenal kumfukuza kocha Mikel Arteta hata kama timu ingeshika nafasi ya kumi na moja. Lakini sasa amekwenda Pre Season na wachezaji wake, ameongeza wengine, unaweza kuanza kumuhukumu taratibu.

Samatta alihitaji Pre Season na wenzake. Alihitaji miezi sita ya kujua mikikimikiki ya Ligi Kuu ya England na kisha aende Pre Season na wenzake kabla ya kupimwa. Naamini atakuwa na msimu bora zaidi lakini hapo hapo tukumbuke kwamba tatizo la Aston Villa halikuwa Samatta peke yake. Timu nzima ilikuwa ovyo.

Lakini hapo hapo lazima tukumbuke kwamba sioni uwezekano wa Villa kumuuza Samatta kwa sababu mpaka sasa Wesley hajarudi dimbani na hata kama akirudi bado itachukua muda mrefu kwake kurudi kuwa fiti na kutamba.

Ni Samatta ndiye ambaye ana nafasi kubwa ya kubadilishana nafasi na Ollie mpaka sasa. Katika mfumo wa kocha, Dean Smith ni wazi kwamba atapenda kuanza na mshambuliaji mmoja. Mshambuliaji huyu anaweza kuwa Ollie kutokana na dau ambalo amenunuliwa lakini kuna mazingira mengi ambayo yatamfanya Samatta acheze na kuonyesha makali yake.

Kwanza kabisa ni mabadiliko ya kawaida ambayo yatamuona Samatta akiingia uwanjani dakika kama ya 60 na kuendelea. Lakini pia kuna nyakati atahitaji kuwaanzisha wote wawili kutokana na mwenendo wa mechi husika.

Kama Villa inahitaji ushindi au sare na wanahitaji kutia nguvu eneo la ushambuliaji huku wakiwa nyuma nadhani kocha atalazimika kuwapanga wote. Lakini pia kuna michuano mingi tofauti ambayo Villa watashiriki na sioni kama watahitaji kutumia washambuliaji watatu tu. Labda kama watanunua mshambuliaji mwingine katika dirisha hili.

Kutakuwa na michuano ya FA, Kombe la Ligi pamoja na Ligi Kuu ya England. Sioni kama kocha atahitaji washambuliaji watatu tu. Labda kama ataongeza mwingine. Akiamua kubakia na washambuliaji alionao basi hapo ndipo watamtambua Mbwana Ally Samatta. Hajawahi kuniangusha.

Naamini kuna vitu vingi amejifunza katika miezi michache iliyopita na akibakia pale sioni mtu ambaye atamnyamazisha Samatta katika kufunga. Kati ya Wesley, Ollie na Davis sijaona mfungaji mahiri kama Mbwana. Namba zake zinaongea. Kwa sasa Watanzania tujifunze uvumilivu tu kwa sababu wengi wanaonekana kukata tamaa bila ya kujua mazingira mapya ambayo Samatta ameingia kwa sasa.