Gwambina, Geita Gold hatumwi mtoto dukani

Muktasari:

Iwapo Gwambina watashinda mchezo huo basi watakuwa wamewaacha wapinzani wao pointi sita, kitu ambacho Geita hawawezi kukubali kupoteza pambano hilo jambo ambalo litakaleza upinzani kwenye mechi hiyo.

BONGE la mechi litapigwa leo pale wababe wa kundi B Gwambina FC watakapokinukisha dhidi ya Geita Gold kwenye pambano ambalo litatoa mwanga mzuri kwa mshindi wa mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Gwambina mjini Misungwi.

Mchezo huo wa Daraja la Kwanza utakuwa na upinzani mkali kutokana na ubora wa vikosi hivyo viwili, huku timu hizo zikiwa zinachuana katika ligi hiyo ambapo Gwambina wana pointi 28 huku Geita Gold wakiwa na alama 25.

Iwapo Gwambina watashinda mchezo huo basi watakuwa wamewaacha wapinzani wao pointi sita, kitu ambacho Geita hawawezi kukubali kupoteza pambano hilo jambo ambalo litakaleza upinzani kwenye mechi hiyo.

Kocha Msaidizi wa Gwambina, Athumani Bilali ‘Bilo’ alisema japo mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanaondoka na ushindi ambao utawafanya waendelee kuongoza katika kundi lao.

Alisema kikosi chao kipo kamili kuwakabili Geita Gold ambapo mchezo huo kwao utakuwa kama fainali kwani ndio utawapa dira katika kundi lao.

Kocha wa Geita Gold, Hassan Banyai alisema wanahitaji pointi tatu katika mpambano huo ambazo zitawafanya wawe sawa na Gwambina FC, hivyo wamejiandaa kikamilifu kuwakabili kwenye pambano hilo.

Alisema pambano hilo ni muhimu kwao kupata ushindi kwani wakipoteza watakuwa wamepishana pointi sita na Gwambina FC, jambo ambalo halitakuwa zuri kwao.