Guinea yaoga manoti baada ya kufuzu Afcon

Muktasari:

  • Ukiachana na kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, Guinea watakutana na Nigeria leo Jumatano katika nusu fainali ya kwanza ya fainali za Afcon.


SERIKALI ya Guinea imewazawadia timu yao ya Taifa chini ya miaka 17 inayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON U17) Dola 3000 zaidi ya Sh6.9milioni kila mmoja baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia baadaye nchini Brazil.

Shirikisho la Soka nchini humo lilieleza kuwa Benchi la Ufundi na wachezaji wote wamepokea zawadi hiyo juzi Jumatatu.

Guinea walifuzu baada ya kupoteza 2-0 dhidi ya Cameroon, kuifunga Senegal bao 2-1 na kuichapa Morocco bao 1-0.

Afisa Habari wa Shirikisho hilo alisema zawadi hizo walipewa kupitia Wizara ya michezo ikiwa kama bonasi yao baada ya kufuzu.

Ukiachana na kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, Guinea watakutana na Nigeria leo Jumatano katika nusu fainali ya kwanza ya fainali za Afcon.

Serikali ya Guinea pia wametoa ahadi ya Dola 5000 kwa kila mchezaji kama timu hiyo itafika hatua ya fainali za michuano hiyo ambayo inafanyika nchini kwa mara ya kwanza.