Guardiola asema kitu kuhusu Juve

Muktasari:

  • Akizungumza baada ya mchezo wa ushindi wa 3-1 iliyopata timu yake mbele ya Watford kwenye Ligi Kuu England, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, Guardiola alizipuuza habari hizo za kuwa anajipanga kuachana na maisha ya Etihad ili akafanye kazi huko Serie A.

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola amesema atakwenda Juventus kama tu atafutwa kazi na Manchester City.

Kocha huyo Mhispaniola amesema hilo baada ya sasa kuwapo na uvumi ameshakubaliana na wababe hao wa Italia kwa ajili ya kwenda kujiunga na timu yao msimu ujao. Taarifa hizo zilidai kocha huyo amekubali ofa ya mkataba wa miaka minne kwenda kurithi mikoba ya Massimiliano Allegri huko Turin.

Akizungumza baada ya mchezo wa ushindi wa 3-1 iliyopata timu yake mbele ya Watford kwenye Ligi Kuu England, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich, Guardiola alizipuuza habari hizo za kuwa anajipanga kuachana na maisha ya Etihad ili akafanye kazi huko Serie A.

Guardiola alisema: “Nina mkataba wa miaka miwili hapa, kuondoka haiwezekani labda kama watanifukuza.

“Kama Manchester City watanitaka, basi nitabaki kwa miaka mingine miwili zaidi, pengine na mingine zaidi. Sioni Juventus kwa misimu miwili ijayo.”

Ushindi huo wa juzi Jumamosi, shukrani kwa hat-trick ya Raheem Sterling imemfanya Guardiola kuendelea kushika usukani wa Ligi Kuu England na kukoleza mbio za kufukuzia ubingwa wa ligi hiyo dhidi ya Liverpool msimu huu.