Guardiola amtumia ujumbe Van Dijk

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA Mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola ametumia ujumbe wa kumfariji beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk baada ya kuumia goti na kulazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Van Dijk huenda akakosa msimu wote baada ya kupata majeraha hayo aliyosababishiwa na kipa wa Everton, Jordan Pickford katika mchezo wa Merseyside Derby uliomalizika kwa sare ya 2-2 uwanjani Goodison Park, Jumamosi iliyopita.

Jambo hilo ni pigo kubwa kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, lakini kocha Guardiola haamini kama jambo hilo litakuwa tatizo kubwa kwa miamba hiyo ya Anfield.

Man City wenyewe msimu uliopita walikumbana na janga kama hilo wakati walipompoteza beki wao wa kati, Aymeric Laporte kwa muda wa miezi minne kutokana na kuumia goti.

Kocha Guardiola alijaribu kumtumia ujumbe wa kumsapoti beki huyo ambaye uwepo wake ni muhimu kwenye ligi.

“Sitaki kuzungumzia namna Liverpool watakavyoathirika. Jurgen atazungumzia hilo,” alisema Guardiola.

“Tunamtakia kila la heri apone haraka. Sipendi timu pinzani ipoteze wachezaji wake muhimu kwa muda mrefu.”