Griezmann keshaaga, mwendo Barcelona

Thursday May 16 2019

 

MADRID, HISPANIA. STAA Antoine Griezmann amewaambia Atletico Madrid ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu huu huku mpango ukiwa kutimkia Barcelona.

Ni hivi, Barcelona baada ya kushindwa kuinasa huduma yake kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, imejiandaa kutumia Pauni 108 milioni kununua mkataba wake kama kinavyojieleza kipengele kwenye mkataba wa staa huyo itakapofika Julai.

Wakali hao wa Nou Camp wanataka kutengeneza kikosi chao kuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao na Griezmann yupo kwenye mipango yao.

Wiki iliyopita kulielezwa kwamba Griezmann ameshafikia makubaliano binafsi na Barcelona na ndio maana amepata nguvu ya kumweleza Kocha Diego Simeone pamoja na Rais wa Atletico, Miguel Angel Gil Marin kwamba anaondoka.

Atletico Madrid ilifichua hilo kwenye ukurasa wake wa Twitter, ikiandika: “@AntoGriezmann ameifahamisha klabu kwamba hataendelea kubaki Rojiblanco msimu ujao.”

Timu hiyo baadaye ilituma video ikimwonyesha mchezaji huyo akizungumza na mashabiki wake ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipotuma video hiyo wakati alipokuwa akiwaambia kwamba hataondoka kwenye timu hiyo.

Griezmann alisema: “Imekuwa miaka mitano yenye mafanikio makubwa kabisa. Nawashukuru kwa kila kitu, mtabaki moyoni mwangu.”

Staa huyo anatarajia kucheza mechi yake ya mwisho kwenye kikosi hicho keshokutwa Jumamosi watakapomenyana na Levante kwenye La Liga. Msimu huu staa huyo amefunga mabao 19 na kuasisti mara 11, huduma ambayo Barcelona inahitaji iwepo kwenye kikosi chake kwa msimu ujao.

Advertisement