Griezmann? Cheki Man United ya kufikirika

Muktasari:

Kwenye safu yake ya ulinzi, Man United imepanga kumsajili kipa Andre Onana kuchukua nafasi ya De Gea kama atakwenda PSG au Juventus huko anakotakiwa, wakati mabeki wa kati inawataka Kalidou Koulibaly na Harry Maguire kuja kucheza beki ya kati, wakati kulia wanamsaka Aaron Wan-Bissaka na kushoto atakuwa Luke Shaw.

MANCHESTER,ENGLAND.MANCHESTER United imekuwa na uhakika itamnasa staa wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann na Mfaransa huyo akitua kwenye kikosi hicho atakwenda kufanya mapinduzi makubwa kwenye kikosi cha kwanza.

SunSport linafichua Man United imeshaandaa ofa ya Pauni 95 milioni ya kumnasa fowadi huyo ili kuanza yale makali yake kwenye usajili katika dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya baada ya kuwashtua mashabiki kwa usajili wa kinda asiyekuwa na jina, Daniel James.

Lakini kuna baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wanaweza kuondoka kwenye kikosi hicho, akiwamo David de Gea, ambaye mkataba wake unafika mwisho na hana dalili ya kusaini dili jipya huku Kocha Ole Gunnar Solskjaer akidaiwa kuchoshwa na Paul Pogba.

Straika Romelu Lukaku, naye anasakwa na Inter Milan, hivyo jambo hilo linaweza kuwafanya mastaa wake hao watatu wenye majina makubwa kabisa wakaachana na maisha ya Old Trafford.

Wachambuzi wa mambo ya soka wameshafahamu namna ambavyo Man United itakavyokuwa msimu ujao kama itafanikiwa kunasa mastaa wake inaowataka.

Kwenye safu yake ya ulinzi, Man United imepanga kumsajili kipa Andre Onana kuchukua nafasi ya De Gea kama atakwenda PSG au Juventus huko anakotakiwa, wakati mabeki wa kati inawataka Kalidou Koulibaly na Harry Maguire kuja kucheza beki ya kati, wakati kulia wanamsaka Aaron Wan-Bissaka na kushoto atakuwa Luke Shaw.

Man United inafahamu itampata Onana kwa Pauni 40 milioni, Wan-Bissaka kwa Pauni 50 milioni huku ikiamini Pauni 150 milioni itatosha kuwanasa Maguire na Koulibaly.

Hapo Chris Smalling, Phil Jones, Eric Bailly, Marcos Rojo na Victor Lindelof itabidi waanzie benchi na wengine watafungulia mlango wa kutokea.

Kwenye sehemu ya kiungo, kwa sababu Pogba anaweza kuondoka, basi Ole amepanga kuwatumia Nemanja Matic na Scott McTominay na kwenye benchi lake kutakuwa na Fred na kiungo mwingine akisajiliwa, wakati mbele yao kutakuwa na Jesse Lingard, kwenye namba 10 ambapo atakuwa akisaidiwa na Juan Mata akisaini dili jipya, wakati kulia atakuwa Marcus Rashford, kushoto ni James na straika ni Griezmann.

Wachezaji kama Anthony Martial, Alexis Sanchez, Fred, Diogo Dalot na Andreas Pereira na wengine ambao watanaswa watakuwa kwenye benchi kuwa na kikosi cha kibabe zaidi.