Gor Mahia mambo ni moto, rungu lawashukia wachezaji

Muktasari:

  • Hata hivyo Oktay kawatetea akiitaja ishu hiyo kuwa ndogo na kumtaka Ambrose aacha kubebana na majungu na wachezaji.

KOCHA wa Gor Mahia, Hassan Oktay ameuomba uongozi wa klabu hiyo kutowaadhibu wachezaji wawili Francis Kahata na Philemon Otieno kutokana na kile kilichotokea Morocco hivi karibuni.

Oktay sasa kawakingia wachezaji wake hao ambao picha zao zilisambaa mitandaoni zikiwaonyesha wakiwa wamelala sakafuni katika Uwanja wa ndege wa Doha, Qatar walipokuwa safarini kuelekea Morocco kwa ajili ya mchuano wa marudiano wa CAF Confederation.

Picha hizo ziliishia kuwatia taabani uongozi wa klabu, ulikashifiwa kwa kutowajali wachezaji wake.

Hata hivyo baada ya kurejea nchini mwenyekiti wa klabu Ambrose Rachier aliitisha kikao na waandishi na kudai kuwa, wachezaji hao walifanya makusudi kuposti picha hizo ili kuchochea hisia za huruma na kuchora taswira kwamba walikuwa wanatesekana na katika hilo kuhakikisha kwamba wameichafulia jina uongozi. Kutokana na hilo Rachier alitishia kuwachukulia hatua kali ikiwemo kusitisha mikataba yao na klabu.

Hata hivyo Oktay kawatetea akiitaja ishu hiyo kuwa ndogo na kumtaka Ambrose aacha kubebana na majungu na wachezaji.

“Jamani haya mambo madogo sio ya kubebana nayo, hakuna familia isiyokosa migogoro na kwa kawaida yatokeapo, husuluhishwa. Tulishayamaliza na wala mimi sina kinyongo na Philemon au Kahata, wala hata sikumbuki kilichotokea kule Doha,” alisema Oktay.

Na kuhusu adhabu ambayo Rachier ameendelea kusisitiza kuwa lazima aitekeleze, Oktay alisema “Tulishazungumza na wachezaji na makosa ni kwa wanadamu kikubwa ni kutorudia kosa hilo. Kikweli hawastahili adhabu yeyote ile hasa baada ya kuwapa msomo mrefu” akaongeza.