Giniki afanya kweli mbio za Uholanzi

Muktasari:

Mwanariadha Giniki alishinda mbio za nusu Marathoni za Kunming Plateu za nchini China, pia ni mshindi wa mbio za taifa za Nyika za kilometa 10 baada ya kushika nafasi ya kwanza akitumia muda wa dakika 28:25.

Arusha. Mwanariadha nyota wa Tanzania, Emmanuel Giniki amefanikiwa kushika nafasi ya pili katika mbio za barabarani kilomita 10 zilizofanyika nchini Uholanzi.

Giniki akiwa Mtanzania pekee aliyewakilisha nchi katika mbio hizo amefanikiwa kutumia dakika 00:27:37 kumaliza mbio zake sekunde kumi na tatu nyuma ya mwanariadha wa Kenya, Davis Kiplagat aliyetumia dakika 00:27:24.

Nafasi ya Tatu ilichukuliwa pia na mwanariadha kutoka Kenya, Issac Kipsang aliyemaliza kilomita 10 kwa kutumia dakika 00:27: 40

Kufuatia ushindi huo Giniki amefanikiwa kutia kibindoni kitita cha dola 5000 (Sh 11 milioni) na kikombe cha rangi ya fedha.