Ghafla tu Pogba na Mourinho wamaliza bifu

Muktasari:

Paul Pogba ameisaidia Manchester United kushinda mechi yake baada kumpa ushauri wa kiufundi Jose Mourinho kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle United.

MAMBO kwisha. Jose Mourinho na Paul Pogba kila kitu kipo sawa unaambiwa, hakuna tena kukwidana mashati kama lisemwalo liko hivyo lilivyo. Wasimuliaji wa mambo ya ndani huko Manchester United wanasema hivi, Pogba alitoa mchango mkubwa wa mawazo ya kiufundi kuisaidia timu hiyo kubadili matokeo ya kufungwa na kisha kuwafunga Newcastle United katika mchezo wa Ligi Kuu England Jumamosi iliyopita.
Unaambiwa hivi, kocha Mourinho baada ya kuona Man United yake imeshachapwa 2-0 hadi mapumziko, walipokuwa kwenye vyumba vya kubadilishia huko Old Trafford, alimfuata Pogba na kumwomba ampe ushauri wa kiufundi kitu gani kifanyike kunusuru mambo kwenye mechi hiyo. Pogba akamwambia Mourinho nini kifanyike kwenye mechi hiyo.
Mourinho aliwapa nafasi wachezaji wengine pia waseme kitu cha kufanya. Kitendo hicho kimeelezwa kiliwafanya wachezaji waone sasa wanaheshimika na kocha huyo na waliporudi uwanjani walikuwa watu tofauti kabisa na ilivyokuwa kwenye kikosi cha kwanza.
Unaambiwa hivi, kwenye kupeana ushauri wa kiufundi, Pogba alimwambia Mourinho yeye arudi nyuma kidogo ili aingizwe Maroaune Fellaini, kitu ambacho Mourinho alilikikubali na kufanya hivyo. Scott McTominay akatolewa kuingia Fellaini. Mwanzoni, McTominay alirudishwa nyuma zaidi baada ya Eric Bailly kutolewa kwenye dakika ya 19 kuingia Juan Mata.
Kwa ushauri wa Pogba, Nemanja Matic akarudi nyuma zaidi kwenye beki, huku kiungo huyo Mfaransa akisimama mbele yao kuwakinga na Fellaini akiwa mbele kupeleka mashambulizi kuwafanya kina Mata kuwa bize kuwashambulia Newcastle.
Mabadiliko hayo ya kiufundi yalimfanya Pogba awe na nafasi kubwa ya kucheza kwenye eneo la kati ya kiwango na kufanikiwa kusawazisha mabao yote na Alexis Sanchez kufunga la ushindi, wakipindua matokeo kutoka 2-0 na kushinda 3-2.
Baada ya mechi Mourinho alisema: “Wakati wa mapumziko tulifungua nyoyo zetu na kuzungumza nini kifanyike kiufundi kama dakika mbili hivyo. Kisha dakika nane nyingine tulizungumza mambo mengine na nadhani hilo liliwafanya wachezaji kujisikia kuwa huru na kipindi cha pili tukafanya matokeo kuwa 3-2. Yani amazing!”
Wakati ikiendelezwa kwamba hali ilikuwa mbaya kwenye vyumba vya kubadilishia, lakini sasa baada ya mechi Man United ilionekana kuwa na muungano mpya. Matumaini mapya yameibuka kwamba huenda huo ndio ukawa mwanzo wa mambo mazuri na mwisho wa malumbano baina ya kocha na wachezaji wake klabuni hapo. Kwa muda mrefu, Pogba na Mourinho wamekuwa wakikabana koo, lakini kwa kilichotokea kwenye mechi ya Jumamosi kwa wawili hao kuzungumza na kushauriana kuhusu ishu za kiufundi. Jumamosi, wawili hao walionyesha kwamba wanaweza kufanya kazi pamoja.
Kinachoelezwa ni kwamba kabla ya mechi hiyo, asubuhi yake, Mourinho alipokea meseji kutoka kwenye bodi kwamba aachane na hizo stori zinazoendelea kwenye vyombo vya habari kwamba atafukuzwa. Haifahamiki kama meseji hiyo ilimtaka pia Mourinho kuwapa nafasi wachezaji wake watoe maoni yao ya kiufundi nini kifanyike ili timu ipate matokeo mazuri uwanjani.
Kuthibitisha kwamba Mourinho kazi yake ni salama, hata Mkurugenzi Mkuu, Richard Arnold alikwenda kumkumbatia Mreno huyo baada ya mechi wakati alipokuwa akifanya mahojiano na vyombo vya habari. Mourinho alikuwa akiulizwa kuhusu hatima yake ndani ya Man United, wakati pembeni yake alikuwapo mtu wa karibu zaidi wa Ed Woodward kiutendaji, Arnold akipita, Mourinho akawaambia waandishi, ‘muulizeni huyo’. Arnold akamkumbatia Mourinho na kusema ‘safi sana’.
Jambo hilo linafuta habari zote kwamba Zinedine Zidane anaweza kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Man United, huku wakala wake Alain Migliaccio akisema hakuna mpango huo.