Generation FC yageuzwa mboga

Muktasari:

 

  • Generation ambayo ilipigiwa upato wa kung’aa katika mchuano huo, ilijipata ikigeuzwa mboga baada ya kushindwa kabisa kukabiliana na kasi ya mahasimu wao ambao walionekana kujiamini katika idara zote.

MATUMAINI ya Generation FC ya kupiga hatua kwenye kinyang’anyiro cha kusaka ubingwa wa Denyenye Soccer Promotion Cup yalifika kikomo juzi Jumamosi baada ya kulazwa bao 1-0 na Eritrea FC katika patashika kali iliyopigwa uwanjani Bamburi Kwale.

Generation ambayo ilipigiwa upato wa kung’aa katika mchuano huo, ilijipata ikigeuzwa mboga baada ya kushindwa kabisa kukabiliana na kasi ya mahasimu wao ambao walionekana kujiamini katika idara zote.

Hata hivyo, baada ya kupigana kufa kupona na kulazimisha sare ya bila kufungana katika kipindi cha kwanza, kipindi cha pili vijana wa Eritrea walirejea uwanjani wakiwa na mbinu tofauti na kuanza kushambulia kama nyuki.

Juhudi zao za kusaka bao muhimu katika mechi hiyo zilizaa matunda dakika za mwisho za mchezo baada ya mabeki wa Generation kukosa kuelewana na kutoa nafasi kwa wapinzani wao kupachika bao hilo muhimu.

Ushindi huo mwembamba uliiwezesha Eritrea kutinga katika hatua ya nane bora na kujiunga na miamba ya Volcano United pamoja na Mkwaju FC ambazo tayari zimejihakikishia nafsi hiyo.

Volcano iliyokuwa imeratibiwa kupepetana dhidi ya Duza FC Jumapili, ilibahatika kufuzu kwa hatua hiyo bila ya jasho baada ya wapinzani wao kushindwa kufika uwanjani.

Hiyo ilikuwa mechi ya pili kukosa kuchezwa katika uwanja huo kwa sababu ya timu moja kukosa kufika uwanjani baada ya vijana wa Mkwaju FC pia kupata ushindi wa chee wapinzani wao, Bodaboda  FC kukosa kufika uwanjani.

Hata hivyo, jambo hilo limekuwa likiwaudhi mashabiki ambao wanalalamika hata baada ya kuacha shughuli zao ili kwenda uwanjani kwa ajili ya kuwapa vijana wao shime wakati wanapocheza, mara nyingi wanapofika kiwanjani wanavunjika moyo wanapopata timu moja ikikosa kufika uwanjani.