Geita Gold yaongeza vita kurudi Ligi Kuu

Muktasari:

Huu ndio ushindi wa kwanza wa Geita Gold kwenye Ligi Daraja la Kwanza ambapo Kocha Hassan Banyai amekiri kuwa zimewapa nguvu upya baada ya mchezo wa kwanza kutoka sare na Arusha FC.

KOCHA wa Geita Gold FC, Hassan Banyai amesema kuwa pointi nne walizokusanya katika mechi mbili za Ligi Daraja la Kwanza katika uwanja wao wa nyumbani zinawapa nguvu kuendelea kupambana kusaka ushindi zaidi na kufikia malengo.

Timu hiyo ambayo ilishushwa Daraja msimu wa 2014/15 kwa kashfa ya upangaji matokeo imerudi Ligi Daraja la Kwanza baada ya kuinunua Mshikamano na kuisajili kwa jina hilo.

Kocha Banyai alisema kuwa licha ya kwamba waliamini kubaki na pointi sita kwenye mechi za nyumbani lakini kwa alama nne walizokusanya si haba na zinawapa morali kupambana zaidi.

Alisema kuwa Ligi Daraja la Kwanza huwa ngumu kutokana na timu zote kufkiria kupanda Daraja,lakini Geita Gold imejipanga vyema kuhakikisha hawaachi kitu.

“Tulijipanga kubaki na pointi sita katika mechi za nyumbani lakini tulishindwa na kuambulia alama nne ambazo hata hivyo si haba na zinatupa nguvu kusaka ushindi zaidi ili kujiweka mazingira mazuri”alisema Banyai.

Banyai aliongeza kuwa kutokana na ushirikiano uliopo ndani ya timu pamoja na mashabiki mkoani humo anaamini Klabu hiyo itafanya vyema na kupanda Ligi Kuu.

Kocha huyo alisisitiza kuwa maandalizi yao hayakulenga mechi za nyumbani pekee isipokuwa waliisoma ratiba hivyo wanajipanga na michezo ya ugenini kuhakikisa wanapata matokeo mazuri.

“Baada ya hapa tunaenda mkoani Mbeya kuwakabili Boma FC na sisi hatujajiandaa na mechi za nyumbani tu,hii ni Ligi kwahiyo iwe ugenini tunapambana kusaka ushindi”alisema Kocha huyo.