Geita Gold, Pamba FC tambo kibaaao

Muktasari:

  • Timu hizo zinakutana Jumamosi ikiwa pande zote zimetoka kupata sare katika uwanja wao wa nyumbani,ikiwa Pamba ilitoshana nguvu na Polisi Tanzania na Geita Gold dhidi ya Green Warrior.

NI mechi ya kibabe unaambiwa, ndivyo unaweza kusema pale timu za Geita Gold FC na Pamba zitakapokutana Jumamosi hii katika uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuwania pointi tatu kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Timu hizo zimepangwa kundi B ambapo Pamba ya jijini Mwanza ndio wanaongoza kwa pointi 10 huku Geita Gold wakiwa nafasi ya pili kwa alama tisa baada ya kucheza mechi tano kila mmoja.

Mchezo huo unatarajia kuwa mgumu na wa upinzani mkali kutokana na kila timu kuwa na hamu ya ushindi ili kuongoza kundi na kujiweka katika mazingira mazuri kwenye vita ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Kocha wa Geita Gold FC, Hassan Banyai alisema mechi hiyo kwake anaiona kama fainali hivyo Pamba wajiandae kisaikolojia kuchezea kichapo.

Alisema mchezo uliopita walifanya makosa na kujikuta wakilazimishwa sare ya bao moja dhidi ya Green Warrior jambo ambalo lilimuumiza kichwa na kwamba mechi hii lazima kieleweke.

“Siwaogopi Pamba licha ya kwamba ni timu kubwa yenye historia, ninachohitaji ni pointi tatu ili kujiweka katika mazingira mazuri, najua ushindani utakuwapo ila nimewaandaa vijana wangu kuhakikisha tunafanya kweli,” alisema Banyai.

Kocha wa Pamba, Juma Yusuph ‘Sumbu’ alisema wanaenda kupambana kusaka alama tatu ili kuendelea kujiweka kileleni kwenye msimamo kundi B.

“Tunaendelea kujipanga kurekebisha mapungufu yaliyoonekana mechi iliyopita, tutapambana kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunashinda,” alisema Sumbu.