Gacheo akabidhiwa mikoba ya Musonye Cecafa

Muktasari:

Cecafa inaundwa na nchi wanachama 12 ambao ni Uganda, Somalia, Kenya, Rwanda, Burundi, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Tanzania Bara, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.

Dar es Salaam. Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limemtangaza Auko Gacheo kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) mpya akimrithi Nicholas Musonye aliyemaliza muda wake.

Mwenyekiti wa Cecafa, Wallace Karia alisema Gacheo amekidhi vigezo walivyoviweka hadi kupewa nafasi hiyo.

"Bodi ya Cecafa ilikaa na kupitia wasifu wa watu walioomba na tukapata majina matatu likiwemo la Auko.

Majina hayo matatu tuliyapeleka CAF (Shirikisho la Soka Afrika) ambao wenyewe ndio wakamteua Gacheo kuwa mtendaji wetu mkuu mpya," alisema Karia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Gacheo alisema kuwa anafahamu kazi ngumu aliyonayo ya kuleta maendeleo ya soka Afrika Mashariki na Kati.

"Nafahamu changamoto zinazoikabili Cecafa hasa suala pa wadhamini na nimejipanga kuhakikisha tunazifanyia kazi.

Jambo la msingi ni kuandaa 'package' (kifurushi) ambacho kitavutia wadhamini waweze kuwekeza katika mashindano yetu," alisema Gacheo