GEORGE MASATU : Bifu langu na Mmachinga lilikuwa hapa tu - 4

Thursday May 16 2019

 

By Mwanahiba Richard

KATIKA sehemu tatu zilizopita za makala haya na beki wa kati wa zamani wa Pamba ya Mwanza, Simba na Taifa Stars, George Magere Masatu, alisimulia masahibu yaliyomfika hadi sasa kuwa dereva wa gari la mizigo wakati alishacheza pia soka la kulipwa kwa miaka saba Indonesia akilipwa mkwanja mrefu.

Katika kuhitimisha leo, Masatu anaeleza pia namna bintie Sandra alivyokuwa kiunganisha cha mawasiliano baina yake na mzazi mwenzie, sambamba na kufunguka bifu lake la straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye kila walipokutana uwanjani ilikuwa lazima zikunjwe. Kivipi? Tiririka naye...!

AMFAGILIA BINTIE SANDRA

Masatu hafichi hisia zake juu ya furaha aliyonayo kutokana na kurejesha mawasiliano na mzazi mwenzie, ambaye walifungiana vioo kwa muda mrefu tangu wakwaruzane.

Mkonge huyo anasema anashukuru mno uwepo wa binti yake Sandra kuwa ni kiunganishi chake na mzazi mwenzie (Mama wa Sandra) ambaye waliotengana na kutokuwa na mawasiliano kwa muda mrefu.

“Kwa sasa kuna mawasiliano baina yangu na mzazi mwenzangu, kutokana binti yetu Sandra anayejiandaa kuolewa kuwa kiunganishi na kurudisha mawasiliano yetu,” anasema Masatu na kuongeza;

“Katika familia kunaweza kuwa na mikwaruzo na hata kugombana, lakini kuwa na mtoto ama watoto ni rahisi kurudisha mioyo na kusahau yaliyopo kwa nia ya kuwasaidia watoto hao kupata furaha, malezi na upendo wa pande zote za wazazi, hili limetokea kwetu pia kwani ni muda hatukuwa na mawasiliano na mwenzangu, lakini sasa yapo.”

BIFU NA MMACHINGA

Kipindi kile wakicheza, Masatu na straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ walikuwa kama chui na paka, kwani kila walipokuwa wakikutana lazima kiwake.

Wachezaji hao walikuwa wakifanyiana undava na wakati mwingine kukunjana uwanjani na kuwapa wakatui mgumu mabeki wenzao kuwaamua, lakini Masatu anafungukia bifu hilo.

Mmachinga anakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya akiwa na klabu ya Yanga aliyoichezea tangu mwaka1993 akitokea Bandari Mtwara hadi 2000 alipoenda Simba na kustaafu 2001.

Straika huyo na Masatu hawakuwa wakiiva, lakini hakuna aliyekuwa anajua lolote kwanini walikuwa wakikwaruzana kila walipokutana uwanjani na Masatu anasema; “Sio kweli kama nilikuwa na bifu na Mmachinga. Ila si unajua mkiwa uwanjani basi jambo lolote baya ama zuri linaweza kutokea, tofauti yetu ilikuwa uwanjani tena wakati tunacheza mechi tu.

“Lakini baada ya hapo kila mmoja aliendelea na maisha yake huku urafiki ukiendelea kama kawaida, tulisahau kilichotokea uwanjani, ilikuwa ni mambo ya soka tu, lakini ni watu ambao mpake leo tuna uhusiano mzuri tu wa kirafiki.”

STARS AFCON 2019

Taifa Stars imefuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Juni mwaka huu huko Misri, na Masatu anaeleza kuguswa na jambo hilo.

“Tunashukuru Taifa Stars imefuzu ingawa kundi walilokuwa wamepangwa halikuwa gumu sana, zamani tulikuwa tunapangwa na timu ambazo kabla hujaingia uwanjani unachanganyikiwa na hatukuwa na maandalizi ya kutosha.

“Tulikuwa tunapangwa dhidi ya timu ambazo tulikuwa hatuzijui maana hakukuwa na utandawazi mkubwa tofauti na ilivyo sasa ambapo kila kitu kipo wazi na ni rahisi hata kujua mbinu za wapinzani.Hiyo imesaidia sana kurahisisha mambo hasa kuwajua wapinzani, wachezaji wanaangalia mikanda ya video ya wapinzani.

“Enzi zetu mara nyingi tulikuwa tunakumbana na mataifa ya Uarabuni ambayo uwezo wao tulikuwa tunaujua siku ya mechi.

“Stars wanapaswa kutambua kuwa wanakwenda kucheza fainali ambazo ni fursa ya kipekee kwao kujitangaza na kujiuza maana pale ni sokoni, ukitisha pale hauhitaji kwenda nje kufanya majaribio.

“Wachezaji wetu wengi wanakwenda kufanya majaribio na wanakwama, hadi sasa sijui wanakwama wapi, huenda wanakwenda bila kujiandaa huku wakiwa na hawajui wanakwenda kuwania nafasi gani, hawaandaliwi kisaikolojia na wale wanaowapeleka pengine nao siyo watu wa mpira.

“Ni jambo baya sana kwa mchezaji kwenda kusaini kwenye timu ambayo hujui utacheza nafasi ipi, matokeo yake wanaozea benchi. Wachezaji wanapaswa kufanya uchunguzi sehemu wanazopelekwa ili wawe na maamuzi sahihi,” anaeleza.

WACHEZAJI WA SASA

Masatu anaelezea kwanini wachezaji wengi wa sasa wanafeli kisoka; “Unajua enzi zetu sisi tulikubali kukosolewa na kufanyia kazi upungufu wetu, hata kuambiana ukweli wenyewe kwa wenyewe, kitu hicho siku hizi naona hakipo kabisa.

“Kila mchezaji ni supastaa, hakuna wa kumsikiliza mwenzake na wengine wanafikia hatua ya kuwa juu ya viongozi wao wa klabu ambao huwalipa, hicho kitu ni kibaya sana kinashusha soka, zamani sisi tulilipwa wote pesa sawa Sh25,000 kila mchezaji na hizo zililipwa kulingana na uwingi wa watu wanaoingia kuangalia mechi.

“Hivyo tulijituma sana ili mashabiki wajae tupate pesa nyingi, sasa hivi hata mashabiki wakiingia wawili lakini malipo ya wachezaji yapo juu, kwanini wasijisahau?”

HANA MZUKA NA MECHI

Anasema hana mpango sana wa kwenda uwanjani kuangalia mechi za Ligi Kuu ama zozote zinazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa kwasababu wachezaji wa zamani hawathaminiwi.

“Nakumbuka kuna siku nilienda kuangalia mechi pale Taifa, cha ajabu nilinyanyaswa sana, nilisukumwa na kupigwa na virungu hata nilipojitambulisha, wachezaji wa zamani mara nyingi hatuthaminiwi pale Taifa.

“Inasikitisha sana kuona TFF inathamini wasanii wa Bongo Movie ambao hawajui hata maumivu ya kulipigania Taifa kupitia soka, wanaingia bure na ulinzi wanapewa kuliko sisi wachezaji. Hawakumbuki wengine tulikaribia kupata ulemavu kwa kulipigania taifa lakini kuingia uwanjani tu ni shughuli kubwa.

“Hivyo huwa naona hakuna haja ya kwenda uwanja kama sina pesa, ni bora nilale ama niangalie kwenye Tv kama nahitaji niione mechi, manyanyaso yamezidi, zamani nilitaka kukatwa mguu kwa ajili ya Taifa leo nipate ulemavu kwa kupigwa virungu, hapana.

“Kikubwa TFF wawatengenezee vitambulisho wachezaji wa zamani ili wapate nafasi ya kuingia uwanjani na kutoa mawazo yao pasipo manyanyaso yoyote,” anasema

KUBADILISHA MAKOCHA

Masatu anasema viongozi wa klabu wanapaswa kuwa na tabia ya kutobadili makocha mara kwa mara kwani inawaathiri wachezaji na kurudisha nyuma ubora wa timu maana kila kocha anakuwa na mfumo wake.

Beki huyo anawataja makocha ambao wametoa mchango mkubwa kwenye maisha yake ya soka kuwa ni Mukhusin Amir, Pius Nyamko wote kutoka Pamba, Mansoor Magram na Abdallah ‘King’ Kibaden akiwa Simba.

“Nimepita kwenye mikono ya wengi, lakini wengi wao wasingeweza kuona ubora wangu bila nguvu ya makocha hao,” anasema.

Advertisement