Francis Cheka amerudi na jambo

Friday October 09 2020
cheka pic

BONDIA bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka amerejea na kuanza mazoezi tayari kurejea ulingoni.

Cheka ambaye alihamishia makazi nchini Msumbiji tangu Desemba 2018, amerejea na kuweka kambi Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

“Nimerudi Tanzania, ingawa maisha yangu yatakuwa Dar es Salaam, nimeanza mazoezi, najifua kwenye kambi ya ngumi iko Chamazi, najiandaa kucheza pambano Desemba, hapa hapa Dar es Salaam,” alisema bondia huyo.

Alisema pambano hilo atazichapa na bondia kutoka nje ya nchini ambaye bado wako kwenye mazungumzo na menejimenti ya Cheka Promotions yatakapokamilika atamuweka wazi.

“Desemba narudi ulingoni, mashabiki wangu wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara kama nimeacha ngumi au la!, Niliamua kupumzika, ngumi hazina kustaafu ndiyo sababu leo hii tunamsikia, Mike Tyson anataka kurudi ulingoni. Bondia huyo mwenye miaka 36 anasema bado ana muda zaidi wa kuonekana ulingoni na kutoa burudani kwa mashabiki wake, ambao waliikosa tangu Desemba 26, 2018 alipochapwa kwa Knock Out (KO) na Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’.

“Bado sijachuja, nimeanza mazoezi ambayo naamini baada ya miezi miwili, nitakuwa kwenye kiwango bora cha kurudi ulingoni,” alisema.

Advertisement

Bondia huyo ambaye alihamishia makazi yake nchini Msumbiji ambako alizaliwa mama yake, alisema ameamua kurudi nyumbani Tanzania alikozaliwa.

Advertisement