Fifa kujadili mgawo wa TFF

Muktasari:

  • Mbali ya fedha hizo, Karia alisema Tanzania itanufaika na Dola za Kimarekani milioni moja zaidi ya Sh 2.5 bilioni za mpango wa maendeleo.

Tanga.SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF) linasubiri kikao cha Kamati ya Ukaguzi ya Fifa ili kutoa uamuzi wa mwisho wa kurejesha mgawo wa fedha za maendeleo uliositishwa kwa miaka minne iliyopita.

Rais wa TFF, Wallece Karia alisema mwishoni mwa wiki kikao hicho cha Kamati ya Ukaguzi ya Fifa (Auditing Compliance) kinafanyika leo Jumanne na ndicho kitakachowasilisha taarifa yake ili kufanyika kwa uamuzi wa kurejesha mgawo huo baada ya kutoridhishwa na matumizi ya fedha jinsi yalivyofanywa.

Alisema ikiwa Fifa itatekeleza maamuzi kama ilivyoahidi kwa Serikali ya Tanzania, TFF itapewa jumla ya Dola 5 milioni zaidi ya Sh 12 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya mgawo wake tangu mwaka 2015.

Mbali ya fedha hizo, Karia alisema Tanzania itanufaika na Dola za Kimarekani milioni moja zaidi ya Sh 2.5 bilioni za mpango wa maendeleo.

Kuhusu ujenzi wa uwanja wa kimataifa jijini Tanga alisema TFF haina nia ya kujenga uwanja wa kimataifa, bali itajenga kituo cha soka ambacho kitakuwa na uwanja wa kukaa watazamaji kuanzia 5,000 hadi 10,000.