Fei Toto, Tshishimbi watibua usajili Yanga

Muktasari:

  • Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Tshishimbi alisema kwa sasa anaendelea na majukumu yake ndani ya kikosi cha Yanga, lakini baadaye ataweka wazi msimamo wake na kitakachofuata.

ACHANA na kiwango bora kabisa alichokionyesha jana Jumanne pale Uwanja wa Taifa kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting, Pappy Kabamba Tshishimbi yuko kwenye rada kali na huenda akaachana na wababe hao wa Jangwani.

Tetesi za Mkongomani huyo ambaye ameanza kurejea kwenye kiwango chake kuachana na Yanga, zimeanza kuumiza vichwa mabosi wa timu hiyo wakati huu ambao, kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiajindaa kwenda nchini England kufanya majaribio kwenye moja ya klabu za daraja la pili.

Fei Toto na Tshishimbi wamekuwa wachezaji muhimu kwenye kikosi cha Mwinyi Zahera, ambapo wamekuwa wakishika eneo la katikati kuzuia na kuchezesha timu na kusukuma mashambulizi mbele.

Habari za kuaminika zinasema kwamba, mkataba wa Tshishimbi unamalizika mwishoni mwa msimu huu na tayari kuna ofa kibao mezani kwake zikiwemo za kumbakiza katika Ligi Kuu Bara na zingine za nje.

Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti, Tshishimbi alisema kwa sasa anaendelea na majukumu yake ndani ya kikosi cha Yanga, lakini baadaye ataweka wazi msimamo wake na kitakachofuata.

“Nina mkataba na Yanga hadi mwishoni mwa msimu na suala la kubaki ama kuondoka hilo nitaliweka wazi baadaye. Lakini, kwa sasa nina ofa nyingi hivyo, ni suala la wasimamizi wangu ambao watanielekeza wapi natakiwa kwenda kucheza soka. Natambua kuwa kuna ofa za hapa ndani na zile za nje, lakini kwa sasa siwezi kuwa na jibu kamili kuhusiana na msimu ujao utakuwa vipi.

“Nimeanza mazungumzo ya mkataba mpya na mabosi wa Yanga, lakini natambua kuwa muda wa kusaka mafanikio na kufika mbali zaidi umefika,” alisema Tshishimbi.

Hata hivyo, alisema kuwa yeye ni muumini mzuri wa fedha na kwamba, yuko tayari kucheza soka popote kama anatimiziwa mahitaji yake muhimu ikiwa ni pamoja na mshahara wa maana ili kumpa mzuka.

“Sijaja Tanzania kumaliza soka langu, hapana, hapa napita tu japo kama itatokea nikapewa dili la maana kwa ajili ya kufanya kazi nipo tayari kubaki hapa. Lakini, ndoto zangu ni kwenda kujaribu kucheza soka nje ya Tanzania ambako tayari kuna ofa na muda ukifika nitaweka wazi. Kwa sasa niache nifanye kazi yangu pale Yanga,” alimaliza Tshishimbi.