Familia MO yafuta mkutano, yaishukuru MCL

Muktasari:

Familia ya bilionea Mohamed Dewji 'Mo' imewashukuru wale wote waliofanikisha kupatikana kwa kijana husasan Rais John Magufuli

Dar es Salaam.Familia ya Mfanyabiashara Mohamed Dewji imefuta mkutano wao wa waandishi wa habari uliokuwa ufanyike leo mchana.

Baba mzazi wa Mohamed Dewji 'MO', Gullam Dewji amesema bado wako katika hali ya furaha na kwamba mkutano huo hautafanyika leo.

Gullam amesema angefurahi wangepata nafasi kidogo ya kumpa muda MO aweze kutulia na kuamua kipi cha kuja kuzungumza.

Amesema mpaka muda huu kijana wake MO anaendelea vizuri ambapo wanataka kumpa muda apumzike huku na yeye akipumzika kutokana na kukosa muda wa kumpumzika wakati wote ambao mwanaye alikuwa haonekani.

Aidha Gullam ameshukuru kazi ya kampuni ya MCL kwa jinsi lilivyofuatilia tukio hili.

"Mkutano sidhani kama tutaweza kuufanya leo tena, tungeomba mtupe nafasi kidogo,” amesema Gullam.

"Nafikiri tutawajulisha kama ilivyokuwa awali unajua Mohamed ametoka katika matatizo vyema akapumzika na hata mimi sijalala unajua.

"Hata hivyo nawashukuru sana jinsi mlivyokuwa karibu nasi wakati wote huu wa hili tatizo, lakini tukitaka kuongea tutawaarifu."