FDL ni presha mwanzo mwisho

Muktasari:

Makala hii inakuletea tathimini ya kile kinachojiri kwenye FDL ambacho bila shaka kinatoa taswira ya moto mkali unaowaka katika ligi hiyo.

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu imefikia raundi ya 13 ambapo timu za Dodoma Jiji FC na Gwambina FC zinaongoza msimamo wa makundi mawili ya ligi hiyo.

Dodoma Jiji FC inaongoza kundi A ikiwa na pointi 27 wakati kundi B vinara ni Gwambina FC ambao wana pointi 25 walizokusanya katika idadi ya mechi 13 ambazo wamecheza.

Raundi nane tisa zimebaki kabla ya ligi hiyo kumalizika na kwa hali ilivyo kuna dalili za wazi zinazoonyesha kuwa huenda ushindani na mvuto wa FDL ukawepo hadi siku ambayo raundi ya mwisho ya msimu itachezwa.

Makala hii inakuletea tathimini ya kile kinachojiri kwenye FDL ambacho bila shaka kinatoa taswira ya moto mkali unaowaka katika ligi hiyo.

Vita ya kupanda

Ni rahisi kutabiri vita ya ubingwa katika Ligi Kuu Bara msimu huu lakini kwa hali ya FDL ilivyo, ni vigumu kutaja timu ambayo inaweza kupanda msimu ujao.

Utofauti mdogo wa pointi uliopo baina ya timu zilizopo juu ya msimamo wa makundi hayo na idadi kubwa ya mechi zilizobakia, inafanya vita hiyo ya kupanda kutokuwa na mwenyewe.

Katika kundi A, timu tano zilizo juu katika msimamo, kila moja ina nafasi na uwezekano wa kupanda ikiwa tu itachanga vyema karata zake. Dodoma Jiji FC inayoongoza, ipo sawa na Ihefu FC ambayo nayo ina pointi 27, wakati nafasi ya tatu, inashikwa na Mbeya Kwanza yenye pointi 25, Majimaji iko nafasi ya nne na pointi 22 huku African Lyon ikishika nafasi ya tano na pointi 21.

Upande wa kundi B, Gwambina FC inayoongoza ikiwa na pointi 25, inazizidi Geita Gold na AFC zilizo nafasi ya pili na ya tatu kwa utofauti wa pointi tatu tu, kwani zenyewe zina pointi 22 kila moja. Gipco na Rhino Rangers kila moja ina pointi 19 kila moja, Mashujaa wana pointi 18 wakati Mawenzi Market wana pointi 17.

Jambo linalokoleza ushindani zaidi ni uwepo wa mechi baina ya timu hizo.

Ukizubaa umeshuka

Kwa mujibu wa kanuni za FDL msimu huu, timu nne zitashuka daraja la kuangukia katika Ligi Daraja la Pili (SDL). Kama ilivyo katika vita ya kupanda, kuna moto mwingine unawaka ambao ni ule wa kuwania kukwepa kushuka daraja ambao huenda ukaendelea hadi mwishoni mwa msimu.

Huku mechi tisa zikibakia, msimamo unaonyesha kuwa takribani timu 18 kati ya 22 zilizopo katika ligi hiyo haziko salama na yoyote ikichemsha katika mechi tisa zilizobaki inaweza kujikuta ikishuka daraja. Hata hivyo kabla ya mechi iliyochezwa baina ya Green Warriors na Sahare All Stars timu za Transit Camp, Sahare, Pamba na Warriors katika kundi B na klabu za Cosmopolitan, Mlale FC, Iringa United na Cosmopolitan za kundi A ndizo zinaonekana ziko katika hatari zaidi.

Kanda ipi kutikisa?

Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zinatawala FDL msimu huu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya timu kwenye ligi hiyo kulinganisha na kanda nyingine.

Hata hivyo licha ya baadhi ya kanda kuwa na idadi ndogo ya timu, bado hakuna kanda yenye uhakika wa kupandisha timu na kwa ushindani ulivyo, zile zenye idadi kubwa ya timu zinaweza kujikuta zimeshindwa kufua dafu mbele ya nyingine zenye chache.

Kanda hizo, timu ilizonazo na pointi ambazo zimekusanya kwenye mabano ni ile ya Nyanda za Juu Kusini inayoongoza ikiwa na timu saba ambazo ni Ihefu (27), Mbeya Kwanza (25), Majimaji (22), Njombe Mji (17), Boma (16), Iringa United (10) na Mlale FC (08).

Dar es Salaam ina timu sita ambazo ni African Lyon (21), Friends Rangers (18), Transit Camp (14), Cosmopolitan(13), Green Warriors (08) na Pan Africa (07).

Kanda ya Ziwa ina timu tano nazo ni Gwambina (25), Geita Gold (22), Gipco (19), Stand United (16) na Pamba (13) huku Kanda ya Magharibi ikiwa na timu za Rhino Rangers (19) na Mashujaa FC (18). Wawakilishi wa Kanda ya Kaskazini ni AFC wenye pointi 22 na Sahare wenye pointi 13 zote zikiwa kundi B, Kanda ya Pwani ikiwakilishwa na Mawenzi Market yenye pointi 17 huku Kanda ya Kati ikiwakilishwa na Dodoma Jiji yenye pointi 27.