Eymael aomba msamaha Yanga, Shikhalo apewa Singida

Muktasari:

Yanga ilipoteza kwa mabao 4-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la Azam.

BAADA ya kipigo cha 4-1 walichokipata Yanga dhidi ya Simba, kocha wa Luc Eymael wa Yanga amesema matokeo hayo lawama ziende kwake.

Akizungumza na Mwanaspoti alisema yeye kama mwalimu anabidi achukue majukumu ya kukubali lawama zote yeye mwenyewe.

"Samahani kwa mashabiki na viongozi wa Yanga, wachezaji hawakuwa vizuri, Morrison hakuwa vizuri lakini muda mwingine ni maamuzi tu ya kocha, dakika 15 za mwanzo na dakika 20 za mwisho tulifanya vizuri lakini hazikutosha kuifunga Simba," alisema.

Eymael alisema ni jambo gumu kuifunga Simba mara mbili mfululizo na alichukua muda kuandaa mbinu zake vizuri ili kuweza kupata ushindi lakini haikuwa hivyo.

"Nimewaambia wachezaji wangu watulie na watambue kwamba wamekuwa huku mimi nikibeba msalaba huu, tunaangalia mchezo ujao," alisema.

Akizungumzia kuhusu kumuondoa katika kikosi cha kwanza kipa wake Faruk Shikhalo licha ya kucheza mechi mbili zilizopita na kutoruhusu goli lolote (Biashara 0-0 Yanga na Kagera 0-1 Yanga), Eymael alisema kumpanga Metacha imetokana na ubora aliouonyesha mazoezini.

"Shikhalo ni mzuri na alikuwa anafanya vizuri mazoezini mpaka Ijumaa, Jumamosi hakuwa vizuri na nilimwambia kabisa kwamba hatocheza," alisema.

Aliongeza kwa kusema licha ya kipa huyo kutocheza mchezo huo, alimwambia atampa mechi ijayo dhidi ya Singida Utd itakayochezwa Jumatano saa 10:00 jioni.