Eymael afichua sababu ya Yondani kusota benchi

Muktasari:

Katika mchezo dhidi ya Simba Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Bernad Morrison, kocha huyo alimpanga mchezaji huyo na kumweka nje mkongwe, Yondani ambaye amejijengia ufalme kwa muda mrefu.

IMANI ya Kocha Luc Eymael kwa Juma Saidi ‘Makapu’ ni kubwa kutokana na uwezo wake wa kucheza mipira ya juu kama alivyofanya kwenye mechi dhidi ya Simba. Makapu ana uwezo wa kucheza kwa ufasaha nafasi ya kiungo mkabaji, beki ya kati na kulia.

“Kila mchezaji naamini ana uwezo wake binafsi, sio kwamba Yondani mchezaji mbaya, lakini katika mchezo dhidi ya Simba tuliwafuatilia kwa muda mrefu na kugundua safu yao ya ushambuliaji ina watu warefu.

“Kuna Meddie Kagere na John Bocco wote vimo vyao vimemzidi Yondani lakini Makapu ni mrefu na alifanikiwa kuokoa hatari nyingi zilizokuwa zinaelekea kwetu, kweli Makapu alistahili nafasi hiyo japo wengi walizoea kumwona akicheza nafasi nyingine,” alifafanua Eymael. Makapu alitua kwenye kikosi hicho kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Shangani ya Zanzibar baada ya Yanga kumwona akiichezea Taifa Stars.

Kocha Eymael ametoboa siri ya kumwamini na kumpa nafasi ya kucheza kila wakati, Makapu katika michezo ya hivi karibuni ndani ya chama lake.

Katika mchezo dhidi ya Simba Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Bernad Morrison, kocha huyo alimpanga mchezaji huyo na kumweka nje mkongwe, Yondani ambaye amejijengia ufalme kwa muda mrefu.

Kuhusu kumbadili namba Makapu, kocha huyo alisema hiyo ni mbinu ambayo huitumia kila wakati na humsaidia kuujua uwezo wa wachezaji zaidi ya namba anayocheza.

“Ona sasa wachezaji wengi wameitwa timu ya taifa ina maana kama ulikuwa huna tabia ya kubadilisha na kuwajenga wachezaji kucheza nafasi kadhaa hapa lazima utafeli hesabu zako.”

Wachezaji wa Yanga walioitwa kwenye timu ya taifa ni Metacha Mnata, Juma Abdul, Makapu, Mapinduzi Balama Feisal Salum ‘Fei Toto’ Ditram Nchimbi ambao wote walianza katika kikosi cha kwanza katika mchezo dhidi ya Simba. Pia, Yondani naye ameitwa kwenye kikosi hicho licha ya kuchezaa dakika tano dhidi ya Simba.