Eti Perez hamjui Paul Pogba ni nani

Muktasari:

Jibu lake limeelezwa inaonekana wazi Real Madrid bado wana mpango wa kumsajili Pogba, hivyo Perez hataki kufunguka sana.

MADRID, HISPANIA . MASIHARA mengine bana. Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ameleta dhihaka akidai hajawahi kumsikia mchezaji anayeitwa Paul Pogba wakati alipoulizwa uwezekano wa kwenda kumsajili kiungo huyo wa Manchester United.

Pogba amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda Real Madrid tangu dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huku Kocha Zinedine Zidane akionekana wazi kutaka saini ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa akakipige Bernabeu.

Hata sasa taarifa hizo za kumhusisha na Man United bado zipo licha ya Pogba kukosekana uwanjani sehemu kubwa ya msimu huu kutokana na kuwa majeruhi. Wakala wake, Mino Raiola amekuwa akilalamika Man United kwa jinsi wanavyombania mteja wake.

Lakini, alipoulizwa kuhusu Pogba baada ya Real Madrid kuwachapa Atletico Madrid na kushinda Spanish Super Cup Jumapili iliyopita, Perez alitabasamu na kusema: “Sifahamu Pogba ni nani.”

Jibu lake limeelezwa inaonekana wazi Real Madrid bado wana mpango wa kumsajili Pogba, hivyo Perez hataki kufunguka sana.

Huko Old Trafford, Kocha Ole Gunnar Solskjaer mara kwa mara amekuwa akisisitiza Pogba bado yupo kwenye mipango yake, licha ya timu hiyo kuhusishwa na viungo kadhaa wa ushambuliaji akiwamo James Maddison, Jack Grealish, Donny van de Beek na Bruno Fernandes, ambaye anapewa nafasi kubwa kufuatia maelezo ameshakubali kujiunga na Man United kama ada itafikiwa makubaliano na Sporting Lisbon. Sporting wanataka Pauni 50 milioni ya kuanzia na nyongeza jingine zitakazofanya dili hilo kufikia Pauni 65 milioni.