Eti, Simba ina nyota 14 tu

Muktasari:

Nyota wa zamani wa Simba, wamesema timu hiyo inahitaji marekebisho makubwa kabla ya kushiriki michuano ya klabu Bingwa Afrika kwa madai kikosi chao sio kipana.

Dar es Salaam. ASILIMIA kubwa ya mashabiki wa Simba wanaamini timu yao ina kikosi kipana, lakini hilo ni tofauti kwa nyota wa zamani wa klabu hiyo waliodai eti Mbelgiji, Patrick Aussems ana nyota 14 tu, huku wengine wakiwa hawama maajabu.
Ipo hivi. Mwaka 2003 Simba ilipofuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwavua taji waliokuwa watetezi, Zamalek ya Misri kikosini kulikuwa na winga matata, Ulimboka Mwakingwe ambaye amekichambua kikosi cha sasa.
Mwakingwe alisema machoni mwa mashabiki wa Simba wanaona timu yao ina kikosi kipana na straika matata Meddie Kagere mwenye uwezo wa kufunga viwanja vyote, lakini kuelekea michuano ya kkimataifa wajiandae kupata presha.
"Kocha Patrick Aussems anawatumia nyota wale wale katika kikosi cha kwanza na sabu yake ni zile zile, angekuwa na kikosi kipana angewapa wakati mgumu wapinzani wake kutojua kikosi cha kwanza, hii ni kuonyesha kikosi si kipana."
"Mimi ni mchezaji na sio shabiki napenda kuzungumzia kiufundi, mfano sasa kila unapopita kwa mashabiki wa Simba utawaona wakiziba jicho wakimanisha Kagere, jina lake linavuma kutokana na udhaifu wa ligi, angecheza na timu kama TP Mazembe na kufanya yake angesifika kweli, lakini ligi yetu dhaifu,"
Kuhusu mabao wanayotambia mashabiki wa Simba, alisema huwezi kuisifu timu kwa vile inacheza na mabeki dhaifu.
"Ukiangalia mabeki wanaokutana nao ni wa aina gani, siwakatishi tamaa ila ukweli ndivyo ulivyo. Kwa kuwa wanaenda kwenye michuano ya kimataifa ambako mabeki hawafanyi makosa kama mabeki wetu, tutajua ubora wa kikosi chetu."