Eti! Sarri akaribia kufunga mabegi yake Chelsea

Tuesday February 12 2019

 

LONDON, ENGLAND.NI maumivu pale Stamford Bridge. Ndani ya dakika 24 juzi Jumapili Chelsea ilikuwa imechezea kichapo cha mabao 4-0. Ndani ya dakika 90 ilikuwa imechezea mabao 6-0. Na kuna watu wawili wametabiri Roman Abramovich ataondoka na kichwa cha mtu.

Wachambuzi wa soka, Graeme Souness na Gary Neville wanaamini kibarua cha kocha Muitaliano, Maurizio Sarri kipo hatarini na muda wowote kocha huyo anaweza kupoteza kazi yake kutokana na fedhea aliyowapa Chelsea juzi.

Souness anadai rekodi za tajiri wa Chelsea, Roman Abramovich dhidi ya makocha wanaofanya vibaya darajani ziko wazi na Sarri anaweza kufuata njia ambayo Muitaliano mwenzake, Antonio Conte alipitia baada ya kumalizika msimu uliopita.

“Sijisikii vizuri kuzungumzia kuhusu makocha kupoteza kazi zao, nimewahi kuwa katika hali hiyo, sio kitu kizuri.

Ukiangalia historia ya Chelsea huwa hawachelewi kufukuza watu katika hali kama hii. Mashabiki wengi wa Chelsea aliokuja katika hii mechi waliondoka wakati wa mapumziko.” Alisema Souness.

“Kwa wamiliki na Wakurugenzi waliokuja, nadhani itakuwa vigumu kwake kuendelea kuwa na kazi hii. 6-0 sio matokeo yanayokubalika kwa Chelsea. Wanaweza kuonekana wana roho mbaya lakini hivyo ndivyo walivyo.” Alisema Souness.

Advertisement

Naye Neville ambaye pia aliwahi kujaribu kazi ya ukocha katika klabu ya Valencia ya Hispania akaishia kufukuzwa alitabiri muda wowote kuanzia sasa unaweza kusikia Chelsea imebadlisha kocha.

“Kwa mahojiano ambayo Sarri ameyafanya unaweza kutoa kwa kumi kwa sababu tunachokisia ni sehemu tu ya hali halisi. Kama mambo yakija hadharani utajua kuwa ndani mambo sio mazuri. Chelsea ni aina ya klabu ambayo usishangae kama utaamka asubuhi na kusikia imebadili kocha.” Alisema Neville.

Kwa mujibu wa mtandao maarufu wa kamari wa Uingereza, Betway, Sarri amepewa alama 2/1 kufukuzwa kazi huku kocha wa Everton, Marco Silva akipewa nafasi kama hiyo baada ya timu hiyo kuendelea kupata matokeo mabovu na ilifungwa wikiendi iliyopita.

Kabla ya pambano dhidi ya City mashabiki wa Chelsea walikuwa na matumaini na timu yao baada ya kuichapa Huddersfield mabao 5-0 mwishoni mwa wiki iliyopita huku wakifuta aibu ya kuchapwa mabao 4-0 na Bournemouth kabla ya pambano hilo.

Na sasa Chelsea imeruhusu mabao 12 bila ya majibu katika mechi zao tatu zilizopita huku juzi wakiruhusu Hat trick ya staa wa kimataifa wa Argentina, Sergio Aguero pamoja na mabao mawili ya Raheem Sterling na moja la Ilkay Gundogan.

Kwa upande wa kocha Sarri mwenyewe alidai bado hajapigiwa simu na tajiri Abramovich kuhusu matokeo hayo lakini atakuwa na furaha kupokea simu yake kwa sababu huwa hawaongei na hajawahi kuongea naye.

“Kama Rais akipiga simu, nitafurahi kwa sababu sijawahi kumskia. Kusema ukweli sijui cha kutazamia.

Sijui kuhusu hali yangu ya baadaye. Inabidi muiulize klabu. Nina wasiwasi na timu yangu, kiwango chetu, lakini kazi yangu siku zote ipo hatarini kwa hiyo sina wasiwasi na hilo, inabidi muiulize klabu.” Alisema Sarri.

Alhamis hii Chelsea itasafiri mpaka nchini Sweden kwa ajili ya kucheza pambano lao la hatua ya 32 bora dhidi ya Malmo, lakini Jumatatu ijayo watakuwa na kibarua kizito wakati watakapocheza na Manchester United katika michuano ya Kombe la FA.

Manchester United imeimarika vilivyo chini ya utawala wa kocha wa muda, Old Gunnar Solskjaer na huenda mechi hiyo ikaamua hatima ya Sarri kama Chelsea itatupwa nje ya michuano hiyo.

Advertisement