Ethiopia Vs Kenya: Tukifanya haya, ushindi lazima

Muktasari:

Mara ya mwisho Harambee Stars kushiriki fainali ya michuano ya Mataifa ya Afrika, ilikuwa ni mwaka 2004 nchini Tunisia, chini ya ukufunzi ya Kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee. Kesho wanakutana uso kwa uso na Ethiopia, katika dimba la Bahir Dar, nchini Ethiopia, wakiwa katika nafasi ya pili katika Kundi F, wakihitaji ushindi wa lazima.

Nairobi, Kenya. Timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, inashuka dimbani kesho, ugani Bahir Dar, nchini Ethiopia, kuwavaa Wahabeshi, wakiwa na nia na ari ya kupata ushindi. Mchezo huo wa Kundi F, ambao ni watatu na  muhimu katika kikosi cha Sebastien Migne.
Endapo watapata ushindi, watajiweka sawa katika kampeni ya kusaka tiketi ya kwenda Cameroon, kushiriki kombe la mataifa ya Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2004, walipofanya hivyo chini ya Jacob ‘Ghost’ Mulee.
Wakati wakielekea mchezo, ni vyema Harambee Stars, inayojivunia kusheheni, maproo 13, akiwemo Nahodha Victor Wanyama anayekipiga katika klabu ya Tottenham Hotspur ya England. Hata hivyo, kuelekea ndoto za kwenda Cameroon, lazima Migne na vijana wafanye haya na ushindi utapatikana tu.
Kufunga goli la mapema
Kila mtu anafahamu kuwa, mbinu bora ya kumuua au kummaliza adui ni kushambulia. Mashambulizi mazuri ambayo yanaweza kuwasaidia ni kupata bao na hata ikiwezekana ni kupata mabao ya mapema. Hii itasaidia kutuliza kasi ya wahabeshi hao.
Michael Olunga na wenzake wapaswa kutumia dakika 15 za mwanzo kumaliza kazi. Hii itasaidia sana, kupata utulivu na umiliki wa mechi, vinginevyo watajikuta wakizidiwa ujanja hasa ikizingatiwa kuwa wahabeshi wana nguvu kubwa ya mashabiki.
Kufunga mianya
Kwa walioshuhudia staili iliyotumika kuimaliza Ghana watakuwa wananielewa. Wacheza filamu wale walifungwa miguu. Licha ya kumkosa Wanyama, Sebastien Migne alihakikisha safu ya kiungo inakuwa imara na kutoruhusu mianya.
Ghana walishikwa wakashikika na hicho ndicho kitakachosaidia pale Bahir Dar. Waethiopia wanatakiwa kufungwa wasifurukute. Wanyama na wenzake wanapaswa kukaba hadi kivuli. Kama itashindikana kushinda basi Sare ni sawa kwani bado kuna nafasi ya kumalizia kazi Kasarani.
Kuepuka dharau
Kama kuna hatari kukifanya katika uwanja wa mapambano ni dharau. Migne na vijana wake wanapaswa kuliangalia hilo. Ni kweli kuwa Ethiopia wanafungika lakini tusisahau kuwa tayari wameshajeruhiwa na hivyo wanahitaji ushindi kwa nguvu zote.
Ethiopia wanaingia katika mchezo huu, wakiwa na nia ya kupata ushindi ili kujiweka sawa katika kampeni ya Kundi F. Katika makaratasi ni rahisi sana kuwafunga Ethiopia kuliko kupata sare na Ghana, lakini uwanjani ni kazi ngumu.
Mara ya mwisho, pande hizi mbili zilipokutana, ilikuwa ni mwaka jana katika mechi ya kirafiki iliyopigwa ugani Kasarani, Jijini Nairobi ambapo licha ya kuonekana kama vibonde kabla ya mchezo, Wahabeshi waliwapeleka puta wenyeji wao na kufanikiwa kulazimisha sare.
Utulivu ni lazima
Unapoenda katika uwanja wa ugenini, kukutana na timu inayoshabikiwa na mashabiki wapatao 80,000, silaha muhimu ni utulivu wa kiakili. Lazima Migne awaambie wachezaji wake kuhusu umuhimu wa silaha hii. Lazima mashabiki wale watawafanyia fujo za kisaikolojia.