Erasto Nyoni : Kiraka wa miaka 13 Stars bado kasi ile ile

Muktasari:

Nyoni, 31, amefunguka kuwa kilichopo nyuma ya kiwango chake ni kujitunza vyema kama mchezaji na kutumia muda mwingi wa zaida kufanya mazoezi.

BAADA ya Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kurejea ikitokea Misri kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’, beki kiraka wa Simba, Erasto Nyoni alitangaza kustaafu kuchezea kikosi hicho.

Mbali na Nyoni, beki mwingine wa Taifa Stars, Kelvin Yondani naye alifuata mkondo wa mkongwe mwenzake huyo la kuachana na soka la kimataifa.

Japo umri umewatupa mkono Nyoni na Yondani, lakini kwenye miguu yao bado wana madini na hilo likawafanya wadau kupaza sauti na kuwaomba kutengua uamuzi huo na kuitumikia Taifa Stars.

Kwa sasa wote wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha wa muda, Etienne Ndairagije, wakiendelea kuuwasha moto kama kawaida.

Hakuna asiyejua uwezo wa Nyoni, ambaye amekuwa akicheza nafasi zote za nyuma, kuanzia beki ya kulia, kushoto, kati na muda mwingine hutumika kama kiungo mkabaji.

Nyoni, 31, amefunguka kuwa kilichopo nyuma ya kiwango chake ni kujitunza vyema kama mchezaji na kutumia muda mwingi wa zaida kufanya mazoezi.

“Soka ndio kazi yangu na ninataka kuifanya kwa muda mrefu zaidi. Najitunza na kufanya mazoezi. Ninapokuwa uwanjani kutekeleza majukumu nafanya kwa umakini na sina kawaida ya kumdharau mshindani.

“Najua uzembe unaweza kuigharimu timu ndio maana wakati mwingine tunafokeana na wenzangu kwa faida ya timu. Huwa nachukia kupoteza mchezo japo ni sehemu ya matokeo ya soka.

“Wasichokijua wengi ni kwamba huyu Nyoni ambaye wanamuona leo anajitunza, wachezaji wengi wanashindwa kucheza kwa kiwango kwa muda mrefu kwa sababu hawajitunzi na hawajitambui,” alisema.

Nyoni, ambaye alitamba kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara akiwa na Azam, maisha yake ya soka yalianza Kituo cha Rolling Stone kisha AFC Arusha kabla ya 2010 kutua kwa Wauza Ukwaju, Azam FC.

Aliichezea Azam FC kwa miaka saba yenye mafanikio makubwa ikiwemo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013/14 tangu kuanzishwa kwake Juni 24, 2007 akiwa na Aishi Manula na John Bocco ambao wote kwa sasa wanakinukisha Simba.

Kutua kwake Simba, ulikuwa ni kama muendelezo kwake wa kuendelea kutwaa mataji wa Ligi Kuu Bara, akiwa na Wekundu wa Msimbazi, alibeba mataji hayo mara mbili kwenye msimu ya 2017/18 na 2018/19.

Nyoni kwenye uchezaji wake soka amewahi kucheza nje ya nchi kama ilivyo kwa wachezaji wengine wa Kitanzania, kiraka huyo mwenye Udambwidambwi mwingi, mwaka 2009 aliichezea Vital’O ya Burundi kabla ya kujiunga na Azam.

Tangu kipindi cha Kocha Mbrazili Marcio Maximo akiwa Stars hadi sasa Nyoni bado anavaa jezi ya Taifa Stars.