Emery afanya mazoezi ya mabeki kujiokoa

Friday November 29 2019

Emery- afanya -mazoezi - mabeki- kujiokoa-kikosi - Arsenal -mabeki-michezo blog-ligi kuu England-EPL-

 

LONDON, ENGLAND . UNAI Emery kwa sasa anapasua tu kichwa namna ya kumaliza tatizo linaloikabili safu ya mabeki ya kikosi chake cha Arsenal baada ya kuonekana kuwa ni majanga makubwa.

Lakini, dirisha la usajili bado sana hadi Januari, hivyo Mhispaniola huyo kwa sasa anachokifanya ni kuhakikisha anafundisha mbinu mpya kwenye safu yake ya mabeki ili kuweka mambo safi.

Katika mazoezi ya hivi karibuni, Emery alionekana kuweka mkazo zaidi kwenye kutengeneza beki ili kupunguza idadi ya mabao wanayofungwa na makosa mengine wanayofanya ambayo yamekuwa yakiwagharimu. Jana Alhamisi, Arsenal walishuka uwanjani kukipiga kwenye Europa League, lakini kabla ya hapo walicheza mechi sita bila ya kuonja ushindi.

Na kubwa linalowatesa kushindwa kupata ushindi ni beki yao mbovu imekuwa ikiruhusu mabao mengi. Kwenye Ligi Kuu England, Arsenal imefungwa mabao mengi kuliko iliyofunga kwenye mechi zao 13 walizocheza. Arsenal imekumbana na mashuti 218 kutoka kwa wapinzani na kwamba inazidiwa na Norwich na Aston Villa kwa timu ambazo zimepigiwa mashuti mengi kwa msimu huu.

Arsenal ilitarajia kukipiga na Eintracht Frankfurt usiku wa jana na kocha Emery anafahamu kwamba piga ua ni lazima apate ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaopigwa Jumapili dhidi ya Norwich City.

Ataendelea kukosa huduma ya mabeki wake Hector Bellerin na Sead Kolasinac na hilo linalompasua kichwa na ndiyo maana amekuwa bize kufanya mazoezi ya kuboresha mabeki wake ili wasifungwe kirahisi.

Advertisement

Na sasa kibarua chake kinahusishwa na makocha wengine kama vile Nuno Espirito Santo wa Wolves, Max Allegri na Mikel Artera, anayemsaidia Pep Guardiola huko Manchester City.

Advertisement