Elias Maguli abanwa karantini

STRAIKA wa FC Platinum ya Zimbabwe yenye maskani yake Zvishavane, Elias Maguri amefichua namna ambavyo anafuatiliwa mazoezi yake binafsi anayofanya nchini humo kutokana na kusimama kwa shughuli mbalimbali za michezo.

Maguri alisema kila baada ya siku nne wamekuwa wakirejesha mrejesho kwa kocha wao kwa kumtumia video ikionyesha muonekano wake na uzito.

“Ni rahisi kustukiwa kama ulikuwa hufanyi mazoezi ipasavyo kwa sababu huenda uzito ukaonekana kuongezeka, ikitokea mfano wiki hii baada ya siku nne labda kuna mchezaji zimeongezeka kilo sita, utaambiwa punguza hizo kwa siku chache tu.

“Hiyo inamfanya mchezaji kujituma, binafsi nimelinda uzito wangu ni ule ule kama ukiongezeka huwa na vipointi au moja ambayo huwa sio shida,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Stand United.

Akizungumzia hali ilivyo nchini humo kutokana na janga la corona linalotikisa dunia, Maguri alisema: “Hali sio mbaya sana huku lakini tunasubiri muongozo wa serikali ndio utaamua.

“Natamani kuendelea na maisha kama mwanzo ili nifahamiane na wachezaji wenzangu vizuri, najiona kumisi kucheza soka.”

Hali itakapokuwa shwari nchini humo ndipo Shirikisho la soka Zimbabwe, litakapotangaza upya tarehe na mwezi ambao Ligi Kuu nchini humo itaanza rasmi kutimua vumbi.