Duh! Huyu Bocco ni balaa

Muktasari:

Ukali wa Bocco umefanya mpaka wadau wa soka kumpigia saluti na kumpa heshima ya kuwa ndiye straika bora wa kizazi hiki baada ya kufikisha idadi ya mabao 131 tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008.

NAMBA huwa hazidanganyi.  Kama unabisha chungulia rekodi ya mabao ya straika na nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ ndio utajua ukweli ulivyo.

Ukali wa Bocco umefanya mpaka wadau wa soka kumpigia saluti na kumpa heshima ya kuwa ndiye straika bora wa kizazi hiki baada ya kufikisha idadi ya mabao 131 tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008.

Rekodi zinaonyesha katika msimu wake wa kwanza tu, mara alipoipandisha Azam Ligi Kuu, straika huyo alifunga bao moja, huku msimu uliofuatia 2009-2010 akafunga (14), 2010-2011 (12), 2011-2012 (19) na kunyakua tuzo ya Mfungaji Bora, 2012-2013 (17), 2013-2014 (7) na timu hiyo ikatwaa ubingwa.

Bocco alikuwa anapanda na kushuka katika ufungaji wake na msimu wa 2014/15 alikuwa majeruhi na alifunga mabao mawili, chati yake ikapanda msimu uliofuata wa 2015/16 (12), 2016/17 (10), 2017/18 (14), 2018/19 (16) na 2019/2020 (7).

WADAU WAMPA SALUTI

Rekodi hizo tamu straika huyo mrefu zimetazamwa kwa kina na wadau wa soka, ambao wameelezea kwa nini ana chati ya kupanda na kushuka, huku wakiona ni mchezaji ambaye amezaliwa na kipaji cha kufunga kilichochanganyika na kupenda kazi yake.

Mchambuzi mahiri wa soka, Mwalimu Alex Kashasha alisema Bocco ni mchezaji bora wa kizazi hiki, akimtofautisha na mchezaji aliyezaliwa kwa kufunga na ambaye anajifunza kufunga.

Alisema Bocco amezaliwa kwa ajili ya kufunga na anaendelea kujifunza namna ya kuwa bora zaidi, jambo analoamini limemsaidia kufikisha mabao hayo.

“Panda shuka ya kufunga kwake inatokana na aina ya wachezaji anaokuwa nao kwa msimu husika, pia kuna kukamiwa baada ya kujulikana ni hatari, ukiachana na hilo kuna kuumia,” alisema Kashasha ambaye kila Jumamosi ana kolamu spesho kwenye gazeti hili akichambua mambo ya soka.

Aliongeza; “Bocco namfananisha na Meddie Kagere, hawana pilikapilika za chenga nyingi sana ambazo zinapendwa zaidi na mashabiki, lakini ni hatari pengine kuliko wenye udamvu udamvu, ukizubaa kuwasoma unashangaa mpira upo ndani ya nyavu.”

Naye kocha mwenye mapenzi na Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema Bocco ni kati ya wachezaji ambao wanajitambua nini wanahitaji katika soka la Tanzania, jambo analoamini limempa mafanikio ya kucheka na nyavu kila wakati ndio maana Simba wamempa unahodha.

“Bocco akiwa fiti kazi inaonekana uwanjani kwani anajua kujipanga eneo la kufunga na sio kila straika ana uwezo wa kufanya hivyo, ndio maana kuna wakati wengine unakuta wanamaliza msimu bila kuambulia kitu,” alisema.

Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema Bocco amelipenda soka nalo halijamwangusha na anaamini ataendelea kufunga na kufikisha idadi kubwa ya mabao.

“Ndio maana akiwa fiti anakuwa anatumika sana ndani ya timu yake na Taifa Stars na kwa aina ya uchezaji wake alipaswa kuwa nje huko,” alisema.

MSIKIE MWENYEWE

Bocco alipotafutwa na Mwanaspoti na kuulizwa juu ya mafanikio hayo akiwa mchezaji mzawa aliyefunika kwenye misimu 10 mfululizo, alisema anaamini nidhamu na kutobweteka ndio sababu ya yeye kufanya kazi bila kuchoka na anapenda kushirikiana na wengine ambao wanamwezesha kufikia mafanikio hayo.

“Uwanja tunakuwa wachezaji 11 hivyo ushirikiano wetu ndio unaleta mafanikio, bado sijafika na naendelea kupambana kuhakikisha nafanya vitu vikubwa zaidi ya hapa nilipofikia,” alisema.

Ukiachana na hilo alizungumzia mafanikio ya ubingwa ndani ya kikosi hicho ilitokana na kuwa na nia moja kuanzia kwa uongozi, wachezaji na mashabiki kuhakikisha wanatwaa ubingwa mara tatu mfululizo.