Dube, Kisu waipaisha Azam FC

Friday October 02 2020
dube pic

Dar es Salaam. Mchango wa mshambuliaji, Prince Dube na kipa David Kisu umehusika kwa kiasi kikubwa kuifanya Azam FC isake kuvunja rekodi yake ya msimu wa 2015/2016, na kuweka mpya ambayo haijawahi kuiweka katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu ilipopanda daraja 2008.

Kwa kuibuka na ushindi katika mechi zake nne za mwanzo za Ligi Kuu msimu huu dhidi ya Polisi Tanzania, Coastal Union, Mbeya City na Prisons, Azam imefanya ibakize mechi tatu kufikia ama kuvunja rekodi yake ya msimu wa 2015/2016, wakati ilipoibuka na ushindi katika mechi sita (6) za mwanzo bila kupoteza au kutoka sare dhidi ya Prisons, Stand United, Mwadui, Mbeya City, Coastal Union na Mtibwa Sugar.

Lakini rekodi mpya ambayo Azam imeiweka ni kupata ushindi bila kuruhusu bao katika mechi nne za mwanzo za Ligi Kuu, ambayo hapo awali haijawahi kuiweka tangu ilipopanda.

Katika msimu huu, Azam ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania, 2-0 mbele ya Coastal Union na baada ya hapo ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 katika kila mchezo, ilipokabiliana na Mbeya City na Prisons.

Hata hivyo, mchango wa Kisu langoni na nyota kutoka Zimbabwe, Dube unaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo, ambayo Azam FC imeyapata katika mechi nne za mwanzo.

Dube anayecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, uwezo wake wa kufumania nyavu na kupiga pasi za mwisho, umemfanya awe mwiba kwa walinzi wa timu pinzani na kuwa chachu ya mabao ya Azam katika mechi hizo za mwanzo.

Advertisement

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 23, amehusika katika mabao manne (4) kati ya matano, ambayo Azam imefunga katika mechi nne za mwanzo. Amefunga matatu na kutoa pasi ya bao jingine.

Lakini si tu kufunga na kupiga pasi za mwisho, Dube ameonyesha uwezo wa hali ya juu wa kumiliki mpira, chenga, kasi pamoja na uamuzi wa haraka pindi awapo au hata asipokuwa na mpira.

Wakati Dube akiwa lulu ya Azam katika safu ya ushambuliaji, upande wa idara ya ulinzi, kipa David Kisu amekuwa mhimili wa timu hiyo katika mechi zote nne za Ligi Kuu alizoichezea.

Kipa huyo ameonyesha kuwa na mawasiliano mazuri na wachezaji wenzake hasa wa safu ya ulinzi, uwezo wa kuokoa hatari zinazoelekezwa kwake, kuokoa mipira ya krosi, lakini pia hesabu sahihi pindi anapokabiliana na mashambulizi ya timu pinzani.

Kisu alisajiliwa na Azam FC katika kipindi cha dirisha kubwa la usajili mwaka huu akitokea Gor Mahia ya Kenya, ambayo aliiongoza kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2018/2019, wakitolewa na RS Berkane ya Morocco kwa kipigo cha jumla cha mabao 7-1.

Wakizungumza na gazeti hili, Dube na Kisu walisema lengo lao kuu ni kuhakikisha Azam FC inafanya vizuri katika mashindano inayoshiriki.

“Nitajitahidi kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha Azam FC inafanya vizuri na kutimiza malengo yaliyowekwa hasa kutwaa ubingwa katika mashindano inayoshiriki,” alisema Dube.

Kipa Kisu aliungana na Dube kwa kusema kiu ya kutaka klabu ifanye vizuri ndiyo imemuimarisha na kumfanya asiruhusu bao katika mechi nne za mwanzo.

“Siri ya mafanikio ni kujituma na kufuata kile ninachoelekezwa lakini kubwa zaidi ni neema za Mungu kwa sababu yeye ndiyo kila kila kitu.

“Nafurahi kuona nafanya vizuri lakini jambo kubwa ambalo linaniongezea ari ni hamu ya kuhakikisha timu yangu inafanya vizuri,” alisema Kisu.

Wakati huo huo, Ligi Kuu inaendelea tena lao, wakati Dodoma FC ikiialika Ruvu Shooting, mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa jamhuri, Dodoma.

 

Advertisement