Dodoma Jiji yaziacha Ihefu, Gwambina FC

Muktasari:

Dodoma Jiji imepanda daraja na kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu.

Dar es Salaam. Wakati hali ikiwa tete kwa timu mbili zinazoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, Ihefu FC na Gwambina FC, Dodoma Jiji ndiyo pekee iliyoonyesha uhai katika raundi tano za mwanzo za Ligi msimu huu.

Na leo wanashuka katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuikaribisha Mbeya City katika mchezo wa mzunguko wa sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Licha ya ugeni wake katika ligi, Dodoma Jiji imeonekana kuanza vyema msimu na kujaribu kujitengeneza mazingira ya kuwa salama tofauti na Gwambina na Ihefu, ambazo zimeanza kwa kusuasua.

Ushindi katika mechi tatu kati ya tano ilizocheza pamoja na sare katika mchezo mmoja, ni matokeo ambayo si tu yameiweka Dodoma Jiji katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi bali pia umeanza kuipa matumaini ya kuingia katika vitabu vya kihistoria kwa kufuata kile kilichowahi kufanywa na Namungo na Singida United katika misimu miwili mfululizo iliyopita.

Katika msimu uliopita, Namungo FC ambayo ndio ilikuwa imetoka kupanda daraja, ilimaliza ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Simba, Yanga na Azam FC, baada ya kukusanya jumla ya pointi 64 ikifunga mabao 46 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 37.

Ukiondoa Namungo FC, KMC ambao walishiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2018/19 walimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo, baada ya kukusanya jumla ya pointi 55, wakifumania nyavu mara 55 huku wakiruhusu jumla ya mabao 25 langoni mwao.

Dodoma Jiji yenyewe ilianza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC, ikawachapa JKT Tanzania 2-0 na ikatoka suluhu na Coastal Union ya Tanga.

Mchezo uliofuata ilikutana na kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania na ikajirekebisha kwa kuitandika Ruvu Shooting 2-0, matokeo ambayo yaliwafanya wawepo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wakiwa na pointi 10, wakifunga mabao matano na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa Dodoma Jiji FC, ndugu zao wawili waliopanda nao, Gwambina na Ihefu SC bado hali ya mambo haijakaa sawa kwa upande wao kwenye mechi tano walizocheza hadi sasa.

Ihefu yenyewe ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi zake tatu ilizokusanya katika mechi tano, ikifunga mabao mawili na kufungwa mabao saba, wakati Gwambina yenyewe ipo katika nafasi ya 14 baada ya kukusanya pointi nne katika mechi tano ilizocheza.

Ikumbukwe kwamba timu nne zitakazokuwa chini ya msimamo wa ligi mwishoni mwa msimu, zitashuka daraja moja kwa moja na wakati huo timu mbili ambazo ni ile iliyoshika nafasi ya 15 na pia nyingine iliyoshika nafasi ya 16 zitacheza mechi za mchujo dhidi ya timu za Ligi Daraja la Kwanza.

Kipa wa Dodoma Jiji FC, Aron Kalambo alisema kuwa bado wana kazi kubwa ya kufanya licha ya kuwepo katika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi.

“Ni jambo jema kufanya vizuri mwanzoni mwa ligi lakini kubwa zaidi tunatakiwa kuwa na muendelezo wa kupata matokeo mazuri ili tuweze kutimiza malengo yetu hivyo tunahitajika kujituma zaidi katika mechi zinazofuata na hatupaswi kubweteka,” alisema Kalambo

Kocha wa Gwambina FC, Fulgence Novatus alikiri timu yake kutoanza vizuri ingawa anaamini itafanya vyema katika michezo inayofuata.

“Muda mfupi timu yangu itasimama vizuri na tutapata matokeo ambayo watu wanayatarajia. Ni ligi ambayo inaonekana ina ushindani. Kuna michezo mingi mbele vipi kama nikishinda yote si tunaweza kuwa mabingwa?

“Inachukua muda kuifanya timu ikasimama lakini kwangu mimi nimeridhika kwamba ndani ya muda mfupi, timu itasimama na tutapata matokeo mazuri,” alisema Novatus.

Katika mchezo wa mapema jana, Gwambina ikiwa nyumbani imeitandika Mtibwa Sugar mabao 2-0 katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Gwambina, mabao ya washindi yalifungwa na Yusuph Dunia kipindi cha kwanza kwa njia ya penalti na Meshack Abraham dakika ya 87.