Dk Msolla, Zahera kusuka mipango ya usajili Yanga

Thursday May 16 2019

 

Katika kuhakikisha Yanga mpya inakuwa moto viongozi wa klabu hiyo wamepanga kukutana na Kocha Mwinyi Zahera ili kuwapa bajeti yake ya usajili.

Awali Zahera alishatangaza ana majina ya wachezaji anaowataka na viongozi walisisitiza wapo tayari kumsajili yeyote anayehitajiwa na kocha wao, lakini jana Mwenyekiti Dk Mshindo Msolla alisema ni lazima kwanza waijue bajeti nzima ilivyo.

“Mtu pekee mwenye jukumu la kufahamu ni kiasi gani kinatakiwa kutengwa kwa ajili ya usajili ni kocha, hivyo tumepanga kukaa na kocha mara baada ya mchezo wetu na Mbeya City ili aweze kupendekeza bajeti ambayo itaweza kusajili kikosi chenye ushindani.”

“Kuhusu kuwa na kamati ya usajili hili pia lipo katika mchakato kwani tayari tumeshateua baadhi ya wanayanga na tunaendelea na mazungumzo nao ili waweze kubeba jukumu la kamati hiyo ambayo ni muhimu sana na tuna imani nao kutokana na kuwa na vigezo vinavyotakiwa,” alisema.

 Pia aliongeza wanatarajia kutumia wachezaji wa zamani kuzunguka mikoani kuangalia vipaji vya wachezaji ambao wanaweza wakasajiliwa kuanzia vijana hadi kikosi cha kwanza na kuweka wazi Zahera mwenyewe hataweza.

 

Advertisement