Dk Mshindo Msolla kemea huu uchafu unaoendelea Yanga

Dk Mshindo Msolla

Muktasari:

Yanga wamefanya uchaguzi wao mkuu hivi karibuni na kumuweka madarakani Dk Mshindo Msolla akisaidiwa na Fredrick Mwakalebela ambaye ni Makamu Mwenyekiti.

Yanga ni moja ya klabu kubwa na kongwe nchini, ina miaka 84 ikifuatiwa na watani wao wa jadi Simba, yenye miaka 83 tangu kuanzishwa.

Ukizungumza Ligi Kuu nchini basi huwezi kuacha kuzitaja Simba na Yanga. Hizi klabu kutokana na ukubwa wake basi huwa zina uwezo wa kufanya jambo kubwa ama dogo hata kama halina maana yoyote basi watu wakalikubali.

Hizi timu zimefanya mambo mengi makubwa katika soka la nchi hii, kuna ya kufurahisha na kuudhi ambayo yote yanabaki kuwa kwenye kumbukumbu za wadau wao.

Hivi sasa Simba ipo kwenye mfumo mpya wa kujiendesha na wameachana na mfumo wa zamani wa kutegemea michango ya wanachama kuendesha klabu yao na sasa ni kampuni, muda si mrefu wataanza kuuza hisa mchakato ukikamilika kabisa.

Simba na Yanga zimeteseka kwa miaka mingi sana kutegemea michango ya wanachama na hawakuwa hata na jeuri ya kutamba kusajili mchezaji wa pesa ndefu lakini sasa wapo huko japokuwa hakuna aliyeweza kusajili mchezaji hata kwa Dola 100,000, ila watafika kutokana na malengo yao.

Yanga ambayo ilikuwa inamtegemea Yusuf Manji miaka ya nyuma alipokuwa Mwenyekiti na mfadhili wao, ilitamba kila kona huku Simba ikitamani mafanikio yao kwani wao kipindi hicho hawakuwa na mtu anayeitwa Mohamed Dewji tajiri anayeiwezesha Simba kwasasa akiwa na mpango wa kutoa Sh 20 bilioni kama mwekezaji.

Mo Dewji ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba tangu uchaguzi mkuu wa klabu ulipofanyika mwaka jana na kutengeneza Bodi ya Wakurugenzi huku Swedy Mkwabi akiwa Mwenyekiti upande wa klabu na alichaguliwa na wanachama.

Yanga wamefanya uchaguzi wao mkuu hivi karibuni na kumuweka madarakani Dk Mshindo Msolla akisaidiwa na Fredrick Mwakalebela ambaye ni Makamu Mwenyekiti.

Sasa basi klabu hizi zinafanya mambo mengi yanayoonwa na jamii. Huko nyuma Simba ilikuwa inafanya ujinga flani kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii hasa wanapotaka kutoa taarifa fulani.

Simba walikuwa wanatumia vibaya ukurasa wao wa Instagram kwa kuweka taarifa ambazo hazijakamilika ama taarifa fulani zilizokaa kiudaku udaku kana kwamba huo ukurasa ni wa mtu binafsi ambaye anajisikia kuweka chochote.

Simba kama wanataka kumsajili mchezaji ama kama wamemsajili tayari basi wataweka picha huku wakiwa wameificha sura yake na kuandika maneno ya kidaku.

Inawezekana aliyekuwa anaendesha ukurasa huo hakuambiwa na viongozi wake kuwa wanataka nini kiwekwe, yeye aliweka taarifa ambazo alipaswa aziweke kwenye ukurasa wake binafsi, ilikuwa ni uendeshaji kurasa wa hovyo.

Hili suala lilipigiwa kelele na viongozi waliambiwa ukweli, ishukuriwe uongozi wa Simba ulipokea na kufanyia kazi upuuzi huo mpaka sasa huwezi kuona kwenye kurasa zozote za Simba zimeweka taarifa ambazo hazijakamilika, hakika wameendana na mabadiliko yao.

Sasa tabia hiyo imehamia kwa watani wao Yanga. Inasikitisha sana kuwa na matumizi mabaya ya kurasa za kijamii za klabu hiyo inayoongozwa na wasomi, watu makini na wanaoelewa nini umuhimu wa kurasa hizo.

Siyo kila kitu wadau wawasitue, mengine ni ya kutafakari kabla hamjayafanya au kama kuna mtu ambaye hajitambui jinsi ya kuendesha mtandao huo ni vyema atafutwe mwingine mwenye utaalamu na uelewa na nini maana ya mitandao ya kijamii inayomilikiwa na taasisi.

Viongozi wa Yanga hebu lizingatieni hili maana mnaweza kuona ni kitu kidogo lakini kinaharibu sura ya klabu kuwa hampo makini na kile mnachokifanya, kwenye hizo kurasa zenu wekeni vitu ambavyo tayari vimekamilika ama kuwa na uhakika navyo.

Inatupa shida kuona kwamba klabu ambazo zina msimu mmoja ama michache tu kwenye ligi ukiingia kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii wanafanyakazi kazi kwa umaridadi mkubwa, hakuna udaku udaku.

Naamini uongozi wa Yanga mtasikia na kuelewa kama walivyoelewa watani zenu Simba huko nyuma na sasa hukuti makosa ya makusudi. Umaridadi na weledi ni kitu muhimu sana kwenye kurasa zenu za mitandao ya kijamii.