Dili za usiku Utd, usajili wa dakika za mwisho

MANCHESTER, ENGLAND. BAADA ya dirisha la usajili kufungwa Oktoba 5, ishu kubwa imekuwa ni usajili wa dakika za mwisho ambao umefanywa na Manchester United kwa kuwasajili Edinson Cavani, Alex Telles, Amad Traore, Facundo Pellistri na Willy Kambwala.

Lakini hii sio mara ya kwanza kwa klabu hiyo kufanya hivyo na baadhi ya wa-chezaji hao walionyesha kiwango kiku-bwa na wengine walishindwa kuonyesha kile ambacho kilitarajiwa na mashabiki wa timu hiyo wakati wanasajiliwa.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya wachezaji waliowahi kusajiliwa katika dakika za mwisho za dirisha la usajili ndani ya kikosi hicho na viwango walivyoonyesha ikiwa pamoja na waliofunika na waliofeli.

Wayne Rooney

Katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka 2004, mchezaji huyu alikuwa anahusishwa kujiunga na United akitokea Everton na dili lake likakamilika katika siku ya mwisho ya dirisha. Rooney ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18, alisainishwa kwa ada ya Pauni 27 milioni. Licha ya kusajiliwa akiwa na umri mdogo mchezaji huyo alionyesha kiwango kikubwa ambacho kiliisaidia sana Man

United. Hadi anaondoka alikuwa ndiye kinara wa wakati wote wa ufungaji akiwa ametupia mabao 253 katika mechi 559. Anafuatiwa na gwiji, Sir Bobby Charlton, aliyefunga mbao 249 katika mechi 758. Rooney alishinda mataji matano ya Ligi Kuu ya England, taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League moja, mataji matatu ya Kombe la Ligi (EFL), Kombe la Dunia la Klabu moja na Kombe la FA moja. Ni miongini mwa wachezaji walioacha historia ya kukumbukwa sana Old Trafford. Kwa sasa Rooney anacheza Derby County ambako anahudumu kama kocha mchezaji. Mkataba wake huko unatarajiwa kumalizika mwaka 2021. na una kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Dimitar Berbatov

Alisajiliwa mwaka 2008 kwa dau la Pauni 31 milioni, kabla ya msimu kuanza.

Kocha wa wakati huo wa Man United, Sir Alex Ferguson aliwahi kukaririwa akisema angetamani kuipata saini ya Berbatov jambo ambalo lilizua mtafaruku kidogo lakini baadaye mchezaji huyo alijiunga nao na msimu wa 2010-11 alionyesha kiwango kikubwa baada ya kufunga mabao 21 katika mechi 42. Huyu pi alionyesha kiwango kikubwa licha ya kusajiliwa katika dakika za mwisho. Ingawa watu wengi hawakutegemea kuona kile alichokifanya kwani hakuwa anatajwa kama mchezaji mzuri sana.

Radamel

Falcao

Matarajio yalikuwa makubwa sana kwa mashabiki wa Man United baada ya usajili wake wa mkopo wa msimu mmoja uliofanyika Juni, 30, lakini mambo yalikuwa tofauti licha ya kuonesha kiwango kikubwa alipokuwa na Atletico Madrid na Monaco. Alifunga mabao manne katika mechi 29 chini ya kocha Louis van Gaal. Mkataba wake ulikuwa na kipengele cha Man United kutakiwa kutoa Pauni 44 milioni kama wangehitaji kumsajili moja kwa moja, lakini hawakufanya hivyo.

Saidy Janko

Mwaka 2013, Manchester United ilitangaza kumsajili mchezaji huyu kutoka FC Zurich akiwa kijana mdogo akitajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza katika eneo la beki na winga wa upande wa kulia. Wakati huo kocha mkuu alikuwa ni David Moyes.

Mchezaji huyo alikuwa kwenye orodha ya wachezaji watatu tu ambao kocha huyo alifanikiwa kuzipata saini zao.

Mambo yalimuendea vibaya katika mchezo wake wa kwanza tu ambao ulikuwa wa Kombe la Carabao, Man United ilikuwa inacheza na MK Don lakini ajabu ikapigway 4-0, huku yeye akionekana kufanya makosa mengi.

Baada ya hapo mwezi mmoja baadaye alitolewa kwa mkopo wa msimu mzima kwenda Bolton na baadaye akauzwa kwenda Celtic.

Marouane

Fellaini

Huyu pia alisajiliwa katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi la mwaka 2013 na kocha Moyes kwa dau la Pauni 28 milioni akitokea Everton. Katika msimu wake wa kwanza hakupata nafasi kubwa ya kuanza akicheza mechi 15, jambo lililosababisha wachambuzi wengi kusema ni miongoni mwa usajili mbovu kuwahi kufanywa na Man United, lakini msimu uliofuatia alionyesha kiwango kikubwa na alikuwa sehemu muhimu ya timu. Hata baada ya Moyes kuondoka, mwamba huyu kutoka Ubelgiji mwaka 2019 aliondoka Man United na kutua Shandong Luneng inayoshiriki Ligi Kuu ya China.

Regan Poole

Huyu anacheza nafasi ya beki wa kati, alisajiliwa mwaka 2015 akitokea Newport County kwa dau la Pauni 100,000 baada ya Man United kushinda vita dhidi ya Liverpool ambayo ilikuwa inamezea mate saini yake na ilimfanyia hadi majaribio. Lakini licha ya kuwahi kuonyesha kiwango kikubwa akiwa na Newport, mchezaji huyo alicheza mechi moja tu tena akiingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Ander Herrera katika mchezo dhidi ya FC Midtjylland ambapo Man United ilishinda kwa mabao 5-1.

Baada ya hapo alitolewa kwa mkopo kwenda Northampton Town kabla ya kurudi Newport County. Poole, 22, kwa sasa anacheza MK Dons ambayo alijiunga nayo msimu uliopita.

DALEY BLIND

Katika dakika za mwisho za dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2014, Man United ilifanikiwa kuipata saini ya beki huyu wa pembeni kutoka Uholanzi kwa ada ya Pauni 14 milioni akitokea Ajax. Lakini katika msimu wake wa kwanza tu alikumbana na shida ya majeraha ambayo yalimfanya akae nje kwa mwaka mzima baada ya kucheza miezi miwili tu, mwaka 2018 Man United ikaamua kurudisha pesa yao kwa kumuuza tena Ajax kwa dau la Pauni 12 milioni. Mchezaji huyo anakumbukwa kwa uwezo wake mkubwa wa kucheza nafasi zaidi ya mbili ikiwa pamoja na beki wa kushoto, beki wa kati na kiungo.

Baada ya kurejea Ajax mchezaji huyo ameonyesha kiwango kikubwa sana hasa katika michuano ya kimataifa ambapo aliisaidia timu hiyo kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa mwaka juzi kabla ya kutolewa na Spurs.

Anthony Martial

Macho ya mashabiki wa Man United yaliwatoka mwaka 2015 baada ya klabu yao kumsajili kijana huyu kwa dau nono la Pauni 58 milioni akitokea Monaco. Jambo hilo liliwashangaza mashabiki wengi kutokana na umri wake na kiasi cha pesa kilichotumika, lakini licha ya kutarajiwa kuonyesha kiwango kikubwa sana, katika siku za mwanzoni Martial hakufanya hivyo ingawa msimu uliopita ulikuwa msimu bora sana kwake baada ya kufunga mabao 23 katika michuano yote.

Martial hadi sasa ni mchezaji ambaye hasomeki kutokana na kiwango kupanda na kushuka mara kwa mara -- Jumapili iliyopita alitolewa kwa kadi nyekundu mapema na United ikapigwa 6-1 dhidi ya Spurs kwenye EPL.